Kampuni ya simu za mkononi, Vodacom Tanzania, wadhamini wakuu wa Ligi
Kuu ya soka Tanzania Bara jana walimkabidhi kitita cha Tsh Milioni 1
kiungo wa Yanga, Thaban Kamusoko baada ya kuibuka Mchezaji bora wa ligi
hiyo kwa mwezi Desemba 2015. Mzimbabwe huyo mwenye rasta kichwani,
aliibuka mshindi baada ya kumshinda mchezaji mwenzake wa Yanga,
mshambuliaji Amiss Tambwe, raia wa Burundi. Kamusoko aliisadia timu yake
ya Yanga kupata ushindi katika michezo iliyochezwa mwezi Desemba kwa
kushiriki dakika zote katika mechi tatu zilizochezwa mwezi huo.
Zawadi ya kitita alikabidhiwa na Mtendaji wa Bodi ya Ligi, Joel
Balisidya wakati timu hiyo ikifanya mazoezi Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam kujiandaa na mechi yao ya Jumamosi dhidi ya APR ya Rwanda Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Katika mahojiano aliyofanya na Vodacom Tanzania, Kamusoko ameishukuru kampuni hiyo kwa kudhamini ligi kuu Vodacom Tanzania na kuwezesha kuonesha kipaji chake pia kwa kumkabidhi zawadi ya fedha taslimu Tsh Milioni 1. Kamusoko amewashukuru pia mashabiki wa timu yake kwa kuendelea kuwasapoti wachezaji na amesema anawapenda na anawaamini sana.
“Ninaimani kila timu inapocheza na Yanga inatamani kutufunga, hivyo
ninawaomba mashabiki wawe wavumilivu, lakini tunawahakikishia ushindi
kila tunapocheza kwenye uwanja huu” amesema Kamusoko.
Naye kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema; “Kwanza
niipongeze timu yote kwa ujumla, na ninaipongeza wahusika kwa sababu
wamemchagua mchezaji ambaye ana vigezo vyote vya kuweza kuwa mchezaji wa
Yanga”
Kamusoko amekuwa msaada mkubwa kwa timu yake ya Yanga akicheza kwa kiwango cha juu.
Note: Only a member of this blog may post a comment.