Mwenyekiti
wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi wilayani Hai (UVCCM),Arnold
Swai amepinga ya kurejea ndani ya chama hicho kwa mwanadiplomasia na
mwanasiasa mkongwe nchini, Balozi Juma Mwapachu.
Balozi Mwapachu, juzi alitangaza kurejea CCM kwa madai ya kuridhishwa na utendaji wa Rais Magufuli.
Akizungumza
na wanahabari jana mkoani hapa,Swai alisema kuwa chama hakipaswi
kumpokea mwanasiasa huyo kwa madai kuwa ni msaliti huku akienda mbele
zaidi na kutaka waliompokea wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa mujibu wa
kanuni za chama.
"Ni
lazima tujiulize, hivi mwanadiplomasia huyo angekuwa tayari kurejea CCM
kama mgombea urais wa UKAWA, Edward Lowassa angeshinda urais?" alihoji na kuongeza:
"Hatuwezi
kumpokea msaliti kama huyu, wakati chama kilipokuwa kwenye mapambano
aliondoka tena kwa kejeli, leo chama chetu kimesimama imara chini ya
mwenyekiti wetu Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ndio anarudi na wimbo
uleule kwamba chama kimemlea, haikubaliki."
Alisema
wakati wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,baadhi ya makada
maarufu wa CCM walikisaliti chama huku wakitoa kauli za kejeli na
kusababisha mpasuko ndani ya chama ambao majeraha yake hayajapona.
Mwenyekiti
huyo alieleza kukerwa na kauli ya Balozi Mwapachu kwamba chama ndo
kimemlea na kwamba hayo si maradhi ya kumuua mtu bali yanatibika, lakini
dhambi ya usaliti haitibiki
"Nguvu
kubwa iliyotumiwa na CCM kuwanadi wagombea wake ilisababishwa na
wasaliti kama hawa,nawaomba viongozi wa ngazi za juu kutofumbia macho
jambo hili kwani ni hatari kwa ustawi wa chama chetu." Alisema
Balozi
Mwapachu alirejea CCM juzi na kupokelwa na mwenyekiti wa CCM kata ya
Mikocheni jijini Dar es Salaam, Athuman Mareenda, ambaye alimkabidhi
tena kadi ya uanachama wa chama hicho.
Note: Only a member of this blog may post a comment.