Siku
chache baada ya kuapishwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
amekuja na mikakati kadhaa ikilenga kubadilisha mwonekano wa jiji hilo
na kulifanya liwe la kisasa.
Miongoni
mwa mambo aliyoyagusia ni usafi, ofisi za Serikali kutokuwa za chama,
kutenga maeneo ya biashara, sensa ya nyumba kwa nyumba, usalama wa raia
na mali zao, watumishi hewa, kurudisha hadhi ya watendaji wa Serikali za
Mitaa, elimu na barabara.
Alitoa
mikakati hiyo jana alipokuwa akizungumza na wenyeviti na watendaji wa
mitaa 559 ya jiji la Dar es Salaam katika mkutano wa kujitambulisha
kwao.
Usafi
Kuhusu
usafi, Makonda alitangaza zawadi ya gari la Sh20 milioni au fedha
taslimu kwa mwenyekiti ambaye mtaa wake utaongoza kwa usafi na Sh5
milioni kwa kila mjumbe wa mtaa husika.
Zawadi hiyo itakayokuwa ikitolewa kila baada ya miezi mitatu, itaanza rasmi Aprili Mosi.
Pia,
aliahidi kutoa pikipiki 30 kwa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam
ili kuwawezesha askari kuwafuatilia watu watakaotupa taka ovyo
barabarani.
“Kampeni
ya kushindanisha mitaa bora kwa usafi itaanza kutakuwa na utaratibu wa
kukutana na viongozi kwa ajili ya kujadiliana mambo mbalimbali ikiwamo
kukabidhi zawadi kwa mwenyekiti atakayeibuka mshindi,” alisema.
Ofisi za Serikali kuwa za chama
Mkuu
huyo wa mkoa ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni, alisema ofisi za Serikali ni kwa ajili ya kazi na siyo sehemu
ya kufanyia siasa akisema katika uongozi wake haangalii chama, bali
kusikiliza matatizo ya kila mtu.
“Ninyi
ni kama viongozi wengine, nataka mtimize ahadi zenu mlizowaahidi
wananchi kipindi cha kampeni siyo kuleta siasa.Tushirikiane kuleta
maendeleo katika jiji hili linalotazamwa na kila mtu,” alisema.
Kutenga maeneo ya biashara
Makonda
alisema matamanio yake ni kuiona Dar es Salaam ya kisasa ambayo itakuwa
na maeneo maalumu kwa ajili ya biashara ya vileo, magari, gereji na
vifaa vya ujenzi.
“Ninatamani kuona Wilaya ya Kinondoni, Ilala na Temeke zikitenga maeneo maalumu kwa ajili ya maduka ya magari na gereji pia.”
Aliwaagiza
wakurugenzi wa manispaa ifikapo Mei Mosi wawe wameainisha maeneo
maalumu kwa ajili ya biashara hizo, huku akitoa mwaka mmoja kwa
wafanyabiashara husika kuhamia huko.
“Kingine wenyeviti kuanzia sasa ni marufuku maeneo ya pembezoni mwa barabara watu kufanya biashara ikiwamo Ubungo,” alisema Makonda.
Alisema
wanaofanya biashara katika maeneo hayo wamekuwa hawalipi kodi hali
inayowaumiza wafanyabiashara wa maeneo rasmi na Serikali kukosa mapato.
Alisema baadhi ya watu wanaofanya biashara katika maeneo hayo wanashirikiana na wenyeviti wa Serikali za Mitaa husika.
Wakati
akiendelea kuzungumzia suala hilo, mmoja wa mwenyekiti alisimama na
kutaka kumpa taarifa lakini Makonda alimkatisha akisema:
“Mkuu wa mkoa akiongea hakuna taarifa, halafu mimi ni mdogo kwenu lakini ndiyo hivyo kiongozi wenu.” Kisha aliendelea bila ya kutoa fursa hiyo.
Alisema
atazungumza na wakurugenzi wa manispaa kuangalia namna ya kuandaa
utaratibu wa kutenga barabara moja kwa kila kata kwa siku moja ili watu
wafanye biashara.
Sensa nyumba kwa nyumba
Makonda aliwataka wenyeviti hao kupita kila nyumba katika mtaa kuorodhesha idadi ya watu wanaoishi na shughuli zao.
“Kwa
kuwapitia nyumba kwa nyumba mtajua watu na shughuli zao hata kuwabaini
wahalifu. Hao ndiyo tunaowatafuta, msiwavumilie watoeni msiogope kufa
kwa kuhofia kuwataja.”
Alisema hiyo itasaidia pia kujua watu wasiokuwa na ajira hivyo kujipanga namna ya kuwasaidia.
Usalama wa raia na mali zao
Makonda
alisema kila mwenyekiti wa mtaa anapaswa kuhakikisha wananchi wake
wanakuwa salama na hilo litafanikiwa endapo atakuwa na utaratibu wa
kujua nani anafanya nini.
Aliahidi
kutoa Sh1 milioni kwa polisi atakayepambana na majambazi, huku milioni
moja nyingine ikienda kwa mtu atakayesalimisha bunduki au bastola kituo
cha polisi.
Watumishi hewa
Akizungumzia watumishi hewa, alitoa agizo: “Nitakapoagiza
orodha ya watumishi hewa ije kamili, kinyume na hapo ofisa utumishi
atalazimika kulipa hata madeni yaliyopita maana anaonekana ana nia ya
dhati ya kufuga uozo huo.”
Hadhi ya watendaji wa mitaa
Makonda
pia aliwaahidi kuwajengea ofisi wenyeviti wote wa Serikali za Mitaa na
kuachana habari za kupanga na kwamba ifikapo Aprili Mosi atawakopesha
pikipiki 1,000 ili ziwasaidie katika utendaji wao wa kazi na kuwasaidia
kujikimu kimaisha.
“Kuanzia
sasa, hakuna mtu kwenda kumuona mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa bila
kuanzia kwa mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa husika ili kurejesha heshima
ya viongozi hawa.”
Elimu
Katika elimu aliwataka watendaji na wenyeviti katika mitaa yao kutafuta wadau kusaidia sekta hiyo badala ya kusubiri Serikali.
Barabara
Kuhusu kero ya barabara, aliahidi kuzishughulikia, huku akiwashangaa wahandisi kwa kukaa ofisini.
Mtazamo wa wenyeviti
Wakizungumzia
maagizo hayo, baadhi ya wenyeviti na watendaji walisema mengi yanaweza
kutekelezeka kwa kuwa mkuu wa mkoa ameonyesha nia katika kuhakikisha
jiji linabadilika.
“Mengi
aliyoyaongea yalikuwa yanafanyika lakini tulikuwa tunakosa msukumo
kutoka juu. Kama ameonyesha nia, hatuna budi kumuunga mkono na kuifanya
Dar es Salaam kuwa mji wa aina yake,” alisema Mwenyekiti wa Mtaa wa Faru – Buguruni, Simba Said.
Mwenyekiti
wa wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Ubaya Chuma alisema watendaji wa
ngazi za mitaa wamekuwa na mengi ya kufanya lakini hawakuwa na fursa
hivyo ujio wa Makonda huenda ukaleta mabadiliko.
Note: Only a member of this blog may post a comment.