HALI ya kisiasa visiwani Zanzibar, inazidi kuwa tete huku siasa za visasi, chuki na uhasama zikionekana kurejea kwa kasi.
Hali
hiyo imejitokeza baada ya ofisi za matawi matano ya Chama cha Wananchi
(CUF) zilizopo Pemba na moja Unguja kuchomwa moto na watu
wasiojulikana.
Matukio
ya kuchomwa moto kwa ofisi hizo yamekuja siku mbili baada ya watu
wasiojulikana kuchoma moto maskani ya CCM ya Sauti ya Kisonge iliyopo
mjini Unguja.
Hata hivyo Jeshi la Polisi visiwani humo limetangaza kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini watu waliohusika na matukio hayo.
Uchomaji huo ulifanyika usiku wa kuamkia jana saa 8 usiku, ambapo watu hao walichoma moto na kuteketeza nyaraka za chama hicho.
Matawi
yaliyochomwa moto ni Kilimahewa mjini Unguja Wilaya ya Magharibi,
Mkanyageni, Kiwapwa, Kiuyu Minungwini, Wingwi na Kinowe yote ya Kisiwani
Pemba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir, amethibitisha kutokeo kwa matukio hayo.
Amesema
kutokana na hali hiyo tayari ameagiza askari wake kuanza uchunguzi wa
tukio hilo haraka ili waliohusika watiwe nguvuni na kufikishwa katika
vyombo vya sheria.
“Ni
kweli kuna hilo tukio ingawa kwa sasa nipo safari kuelekea Unguja na
tayari nimeagiza kuanza kwa uchunguzi wa matukio haya ili wahusika
waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“…siwezi kusema kama matukio haya yana uhusiano wa masuala ya kisiasa ingawa huu ni uhalifu kama uhalifu mwingine,” alisema Kamanda Nassir.
Akizungumzia
tukio hilo, Mbunge wa Wingwi, Juma Kombo Hamad (CUF), alilaani tukio
hilo huku akiwatuhumu wafuasi wa CCM kuhusika nalo.
Alisema hatua ya CUF kutangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu imekuwa ikiwaumiza CCM.
“Haya
mambo yapo wazi tumeumizwa vya kutosha lakini katika hilo mimi binafsi
wala sifichi hapa kuna mkono wa CCM na sisi hatutarudi nyuma
tunaendelea na msimamo wa chama,” alisema Hamad.
Kauli ya Maalim Seif
Machi
4, mwaka huu, Akizungumza na wafuasi wake waliomtembelea nyumbani
kwake, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema yuko
tayari kukamatwa kutokana na msimamo wake wa kutotambua uchaguzi wa
marudio.
“Msidhani
kuwa mtatupiga shavu la kulia tukawageuzia la kushoto. Kila mara
tunaibiwa, tunapigwa, tunafanywa kila kitu. Tukisema kuwa watu
wajilinde, inakuwa nongwa.
“…basi
tunawaambia kuwa kuitwa polisi, kuwekwa ndani, kufunguliwa mashtaka ya
bandia, hata kuteswa, hayo ni mambo yamekuwa yakitutokea tangu 1992
tumeshayazoea,” alisema Maalim Seif.
Alisema
udhalilishwaji kama huo haujawahi kukirudisha nyuma chama chake, zaidi
ya kukiongezea umashuhuri na ufuasi mkubwa visiwani Zanzibar, huku
akilituhumu Jeshi la Polisi kwa kuwa ‘tawi la CCM’ ambalo litakuwa
dhamana wa machafuko yoyote yatakayotokea.
Katika
hatua nyengine, Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais katika
Uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana alirudia msimamo wa chama chake wa
kutoshiriki kile alichodai uchaguzi wa marudio ulioitishwa na Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha, Machi 20, mwaka huu.
Alisema yeye alishashiriki uchaguzi na kushinda na hahusiki kabisa na uchaguzi mwengine. “Ninamwambia Jecha kuwa uchaguzi huo ni wenu peke yenu,” alisema Maalim Seif.
Note: Only a member of this blog may post a comment.