Papa Francis na mgombea wa Republican mwenye matamshi tata, Donald Trump wameingia kwenye mvutano kuhusu ukristo wa mgombea huyo kufuatia matamshi yake kuwa akichaguliwa kuwa Rais wa Marekani atajenga ukuta mpakani mwa Mexico na Marekani ili kuzuia wahamiaji kuingia nchini humo.
Trump alieleza hivi karibuni kuwa atachukua hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya jitihada za kulinda usalama wa Marekani ikiwa ni pamoja na kuzuia Watu wenye imani ya Kiislamu kuingia nchini humo.
Kauli hiyo ya Trump imeonekana kumkwaza Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ambaye amesema kuwa mtu anayepanga kujenga ukuta kati ya Marekani na Mexico badala ya kujenga daraja ‘sio Mkristo’.
“Mtu anayefikiria kujenga ukuta, kokote walipo, na sio kujenga madaraja, sio mkristo. Hii sio injili,” Papa Francis aliwaambia waandishi wa habari.
Trump amejibu kauli hiyo ya Papa akieleza kuwa Kiongozi huyo hana haki ya kumhukumu mtu yeyote kuwa ni Mkristo au sio Mkristo.
“Hakuna kiongozi, hususan kiongozi wa dini, mwenye haki ya ya kuhoji imani ya kidini ya mtu mwingine,” Trump alisema.
“Kama Vatican itashambuliwa na ISIS, ambapo kila mmoja anajua kuwa ni tuzo muhimu ya ISIS, ninawaahidi kuwa Papa atatamani na kuomba kuwa Donald Trump angekuwa Rais,” aliongeza Trump.


Note: Only a member of this blog may post a comment.