DAR ES SALAAM! Kumbe kuchepuka
hakuna umri bwana! Mwanamke ambaye jina linapigwa ‘tinted’ kwa sasa,
Ijumaa iliyopita alinaswa akiingia kwenye gari la mwanaume
anayedaiwa ni mchepuko wake na kwenda kusikojulikana baada ya
kufuatiliwa kwa karibu na shemeji yake akishirikiana na makamanda wa
kikosi maalum cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ cha Global Publishers,
lisikilize Amani.
ENEO LA TUKIO
Tukio hilo la ‘aibu yake’ lilijiri saa 6:00 mchana wa siku hiyo kwenye maegesho ya maduka makubwa ya Mlimani City jijini Dar.
SIMU OFM
Ilikuwa saa 5:17 asubuhi, simu iliingia
kwenye chumba cha habari ambapo mpigaji alisema yeye anaitwa Dadi.
Alisema ana shemeji yake (mke wa kaka yake) amekuwa akichepuka sana,
hasa kipindi hiki ambacho kaka yake amekwenda kikazi nchini Marekani.
SIKIA SIMULIZI
“Huyu shem, karibu kila siku anachepuka.
Na akitaka kwenda kwenye michepuko yake inaanza kuingia simu, akiongea
utasikia ‘i miss you’, ‘me too honey’. Baadaye anauliza ‘wapi’, ‘basi
nakuja sasa hivi’. Halafu anajiandaa na kuondoka. Mi inaniuma sana kwani
bro (kaka) ameacha pesa ya kutosha na ikibidi huwa tunakwenda kuchukua
kwenye biashara zake, Sinza (Dar).
“Sasa leo muda huu, kapokea simu.
Nikamsikia akisema najiandaa sasa hivi. Nitapanda Bajaj hadi pale nje
Mlimani City, nitaingia na geti la barabara kubwa. Nitakupigia.
“Jamani kama kweli ninyi ni OFM, naomba
tukutane pale muda huu, ndiyo ametoka kama dakika tano tu. Mi naumia
sana. Nimemuuliza safari ya wapi shem, akasema anakwenda kwenye Vicoba,
lakini mi najua hana cha Vicoba wala vifurushi,” alisema shemeji mtu
huyo.
OFM YAJIPANGA
Baada ya maelezo hayo, OFM walijiteua, baadhi ya makamanda walikwenda Mlimani City na kukutana na Dadi ambaye alisema:
“Naamini hajafika, ila sasa kwa sababu
atashuka nje ya geti, sisi tukaeni humuhumu ndani, akiingia
nitawaonesha. Mi naumia sana kwa kweli. Bro akijua hakuna ndoa tena.”
BAADA YA DAKIKA 20
Zilipokatika dakika 20 huku OFM na Dadi
wakirandaranda ndani kwenye maegesho, jamaa huyo alimwona shemeji yake
akiingia kwenye geti linalotazamana na Barabara ya Sam Nujoma.
“Eheee! Yule anakuja, amevaa t-shirt na suruali ya kitambaa chenye mauamaua,” alisema shemeji mtu.
OFM YATEGA KAMERA
Kwa vile Dadi alisema haoni sababu ya
kumfumania shemeji yake kwa kuwa yeye si mume. Aliomba apigiwe picha za
kumwaga ili iwe ushahidi siku likitokea la kutokea.

Ilibidi OFM wajipange mara tatu. Mmoja
alikaa ndani na kamera ya kuvuta kwa mbali, wa pili alikwenda kusimama
geti aliloingilia mwanamke huyo na wa tatu alitoka nje na kwenda
kusimama kwenye geti la kutokea kwenye Baa ya DDC.
Mwanamke huyo, aliingia kwenye gari aina
ya Toyota Prado ambapo dereva wake alikuwemo ndani kwa muda kisha
wakaondoka kupitia geti la kwenye Baa ya DDC. Lilikata kulia na kushika
mzunguko wa magari kwa kuelekea Mwenge.
MASWALI NA DADI
OFM: “Wewe una uhakika gani kama yule ni mchepuko wa shemeji yako?”
Dadi: “Shemeji hafanyi
kazi, hafanyi biashara. Yule ni nani sasa? Japokuwa sijamwangalia
sawasawa kwa sababu nilijificha lakini simjui. Na kama kweli alikuwa
anakuja kwenye Vicoba kwa nini wametoka hata bila kukaa kule kwenye
meza?
OFM: “Kawaida akitoka muda huu huwa anarudi saa ngapi nyumbani?”
Dadi: “Nne, tano usiku, tena akiwa amelewa chakari.”
OFM: “Mnaishi wapi?”
Dadi: “Sinza, Mugabe.
Yaani mtaani ni aibu tupu. Kila mtu anajua shemeji yangu mchepukaji.
Namwomba Mungu bro arudi salama akutane nayo mwenyewe.”
MADAI YALIVYO
Kumekuwa na madai kwamba, eneo hilo la
maegesho ya Mlimani City hutumiwa na watu wenye kuvunja uaminifu wa
kimapenzi. Wengi huingia humo na kuwasubiri wanaochepuka nao kisha
kuondoka badala ya kuwasubiri mitaani.
Imeandikwa: Chande Abdallah na Boniphace Ngumije.


Note: Only a member of this blog may post a comment.