Stori: Mwandishi Wetu, UWAZI
Mfanyabiashara
mkubwa jijini Dar aliyepandishwa Mahakama ya Kisutu jijini Dar wiki
chache zilizopita kwa mashtaka ya kujipatia mali zinazodhaniwa kuibwa au
kupatikana kwa njia isiyo halali, Daudi Yakubu Adam ‘Kanyau’(46),
ameendelea kusota kortini baada ya kesi yake kuhairishwa tena kwa
upelelezi kutokamilika.
Kanyau anayetuhumiwa kwa makosa hayo
yanayotajwa kuwa kinyume cha sheria namba 16, kifungu cha 312 (1) (b) ya
mwaka 2002, kesi yake iliahirishwa kwa mara ya kwanza Februari 3, mwaka
huu na kupangwa kusikilizwa wiki iliyopita yaani Februari 17, mwaka
huu.
Kigogo huyo ambaye alipopandishwa
mahakamani hapo kwa mara ya kwanza wiki chache zilizopita alikuwa mtata
kwa kuwazuia waandishi wa gazeti hili kumfotoa, zamu hii alikuwa mtulivu
huku muda wote aliokuwa eneo la mahakamani hapo alivalia mawani myeusi.
Hata hivyo, mara baada ya habari ya
Kanyau kuandikwa, kupitia mawakili wa Kampuni ya Brocard Attorneys ya
jijini Dar waliliandikia Gazeti la Uwazi barua wakidai fidia ya shilingi
milioni 500 kwa madai kuwa habari hiyo ni ya uongo kwani mteja wao
hakuwahi kutuhumiwa, kukamatwa na polisi wala kufikishwa mahakamani.

Note: Only a member of this blog may post a comment.