BAO la straika wa Yanga, Amissi Tambwe alilolifunga wikiendi iliyopita kwenye mchezo wao dhidi ya Simba, limemfanya aifikie rekodi ya wakongwe wawili wa Yanga, Dua Said na Said Sued ‘Scud’.
Rekodi hiyo aliyoifikia Tambwe ni ile ya kuifunga Simba bao katika mechi zote mbili za ligi za msimu mmoja.
Kwenye mchezo wa raundi ya kwanza uliopigwa Septemba 26, mwaka jana, ambao Yanga ilishinda mabao 2-0, Tambwe raia wa Burundi alifunga bao moja na pia akafanya hivyo wikiendi iliyopita kwenye ushindi wa mabao 2-0.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Mei 18, 1991, timu hizo zilipokutana na Yanga kuondoka na ushindi wa bao 1-0, Scud alifunga bao pekee na waliporudiana Agosti 31, 1991, Yanga pia iliibuka na ushindi kama huo mfungaji pia akiwa Scud.
Hii ina maana kuwa Tambwe ameingia kwenye rekodi nyingine katika klabu hiyo ya Jangwani akiwa aliachwa na kikosi cha Simba kwa kile kilichodaiwa kuwa ameshuka kiwango.

Note: Only a member of this blog may post a comment.