Thursday, November 12, 2015

Anonymous

U.T.I JANGA LISILOPEWA KIPAUMBELE-2

Wiki ya jana nilianza kulielezea tatizo la U.T.I (Urinary Tract Infections) na nilieleza kuwa hili ni tatizo la maambukizi katika njia ya mkojo ambalo huwasumbua watu wengi siku hizi. Uambukizi huu unaweza kusababisha maumivu na kukosa raha. Pia nilieleza kuwa U.T.I ni ugonjwa ambao huwaathiri zaidi wanawake ukilinganisha na wanaume na sababu kubwa ikiwa ni ya kimaumbile, ingawa kuna sababu nyingine kama kufanya ngono na historia ya kifamilia.

Pia nilieleza U.T.I husababishwa kwa kiasi kikubwa na bakteria ambao huingia katika mrija wa kutoa mkojo kutoka katika kibofu. Asilimia kubwa ya ugonjwa huu katika jamii husababishwa na bakteria ajulikanaye kama Escherichia Coli (E Coli), Pia asilimia ndogo yaweza kusababishwa na aina nyingine ya bakteria ajulikanaye kama Staphylococcus Saprophyticus.

Leo ningependa kukujuza pia watoto wanaweza kuathirika na ugonjwa huu wa U.T.I, hususan watoto wa kike walio chini ya umri wa miaka miwili na watoto wa kiume wasiotahiriwa. Dalili kuu kwa watoto wenye ugonjwa huu ni homa, ingawa vipimo huhitajika ili kuhakikisha uwepo wa ugonjwa. Wazee nao pia huweza kuathirika na ugonjwa huu.

Kama nilivyoelezea awali kuwa maambukizi haya katika mfumo wa mkojo ndiyo kitaalamu huitwa U.T.I. Mfumo wa mkojo unahusisha sehemu kuu nne:-

Figo (Kidney), ambazo ni ogani zilizo na umbo la punje za maharage na zinakuwa mbili, ukubwa wake ni kadirio la unavyokunja ngumi yako. Kazi ya figo ni kuchuja damu na matokeo yake ni mkojo unaotengenezwa na hutolewa kama uchafu mwilini.

Mirija ya kutoka figo kwenda kwenye kibofu (Ureters), huwa ni miwili na hupeleka mkojo kwenda kwenye kibofu.
Kibofu ambacho kazi yake ni kukusanya na kuhifadhi mkojo unaotoka katika figo, hutolewa pale mtu anapoamua kukojoa.

Mrija wa kutoa mkojo kutoka kwenye kibofu (Urethra), huu ni mrija mmoja ambao hutoa mkojo nje mtu anapoamua kukojoa.Ugonjwa huu ambao hauko katika kundi la magonjwa ya zinaa, lakini kufanya ngono wakati mwingine husababisha kuambukizwa kwa ugonjwa huu.
Usikose kufuatilia mada hii Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.