Marehemu Maulidi Shaban enzi za uhai wake.
Suzan Kayogela na Chande Abdallah INAUMA SANA! Kijana mmoja
aliyefahamika kwa jina la Maulidi Shaban (21) ameuawa kwa kuchomwa kisu
na rafiki yake aliyetambulika kwa jina moja la Dotto (16) mkazi wa
Kigogo jijini Dar, kisa kikiwa ni CD ya filamu aliyomkodisha. Tukio hilo
lilitokea Novemba 10 majira ya saa tatu usiku eneo la Kintiku ambapo
Maulidi alikuwa na kibanda cha kuuza na kukodisha CD. Chanzo chetu
kilielezwa kuwa kijana huyo aliuawa kikatili baada ya kumshtakia Dotto
kwa bibi yake kwa kutolipwa pesa wala kurudishiwa CD yake. 
Mtuhumiwa wa mauaji hayo.
“Alipofika nyumbani kwao alimkuta bibi yake Dotto na kumwambia kila
kitu na alipoondoka majira ya usiku ndipo Dotto na rafiki yake
walimfuata Maulidi kibandani kwake na kumtishia kisu. Alipotaka kukimbia
ndipo rafiki yake Dotto anayetajwa kwa jina la James alimpiga mtama na
kuanguka hapo ndipo alipochomwa kisu. “Watu walijitokeza kumpa msaada
kwa kumpeleka kituo cha polisi maana alikuwa amejeruhiwa kifuani na
mkononi, hali yake ilikuwa mbaya sana na alipokimbizwa Hospitali ya
Amana, walipewa rufaa kuelekea Hospitali ya Muhimbili lakini alifariki
akiwa anapatiwa matibabu,” kilisema chanzo hicho. Akizungumza na
mwandishi wetu, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kigogo Kati, Ibrahim Said
alisema tukio hilo limewafikia na tayari kesi imefunguliwa katika Kituo
cha Polisi Magomeni na upelelezi unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwasaka
watuhumiwa. 
Mwili wa marehemu ulisafirishwa kuelekea mkoani Tanga kwa mazishi. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.
Note: Only a member of this blog may post a comment.