Miili ya watu wawili waliokufa maji baada ya kusombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha mwanzoni mwa wiki hii jijini Mwanza, ukiwamo wa mwanafunzi, imeopolewa kwenye mwalo wa Ziwa Victoria.
Matukio hayo yalitokana na mvua hizo zilizonyesha Novemba 2, mwaka huu kwa saa tano huku zikiharibu miundombinu, mali na nyumba kujaa maji.
Mkumbo alisema miili hiyo iliopolewa kwa ushirikiano wa polisi na wananchi na kwamba ilikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko.
“Wakati wanatoka hapa (nyumbani) mvua haikuwa kubwa, ila waliondoka wamevaa nguo za nyumbani, zile za shule waliziweka kwenye mfuko ili zisilowane kabla hawajafika shuleni. Inasemekana aliteleza kwenye daraja akaanguka, akaanza kupiga yowe kuomba msaada,” alisema Alex.
Alisema kutokana na muda huo mvua kuwa iliendelea kunyesha, hakuweza kupata msaada hadi mwenzake alipokwenda kutoa taarifa shuleni.
Mkuu wa Sekondari ya Nyamanoro, Praxeda Kaijage alisema walipata taarifa hizo kwa mwanafunzi huyo baada ya kufika shuleni hapo.
Alisema baada ya kutoa taarifa kwa walimu, walianza kufuatilia kwa kushirikiana na familia yake. “Tulipewa taarifa na mwanafunzi mwenzake aliyekuwa naye (Asnaty) kuwa ameteleza kwenye daraja, akachukuliwa na maji, tulichukua hatua haraka kwenda eneo la tukio ila hatukuona kitu, tulifanya jitihada za kuwasiliana na familia tukawa tunamtafuta ila hatukufanikiwa,” alisema Mwalimu Kaijage.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyamanoro Kaskazini, Shija Salileje alisema waliitisha mkutano na kushirikiana kumtafuta mwanafunzi huyo kwenye mitaro hadi ziwani. Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga alisema licha ya kutoa boti mbili, waliagiza watendaji wa kata, mtaa na wenyeviti kumtafuta mwanafunzi huyo na kuhakikisha anapatikana.


Note: Only a member of this blog may post a comment.