Shoga yangu, kwa uweza wa Jalia ni matumaini yangu kwamba hali yako ni nzuri na unaendelea kupambana na maisha kwa sababu bila kufanya hivyo ni wazi utakwama na kujikuta ukiishia kuwa ombaomba jambo ambalo siyo zuri.
Kwa upande wangu nipo bukheri wa afya na nipo ofisini nakuandalia mada ya wiki ijayo lengo likiwa lilelile la kupeana elimu ya uhusiano na kukosoana pale inapotokea wenzetu wanakwenda ndivyo sivyo.
Leo shoga yangu nimekuandalia mada inayohusu kumtoa ‘out’ mumeo, mchumba au mpenzi wako kwani ni suala ambalo baadhi ya wanawake hawajui umuhimu wake katika kuboresha penzi lao.
Nasema hivyo kwa sababu baadhi ya wanawake wanafikiria mwenye jukumu la kumtoa out mkewe, mchumba au mpenzi ni mwanaume, huko ni kukosea kwani kitendo cha wanaume kupewa ofa ya kwenda matembezi na wenza wao kinawapa raha sana.
Shoga yangu, kumtoa out mtu wako kunaimarisha penzi lenu na kumfanya kila mmoja wenu kuwa karibu na mwenzake badala ya kuwafikiria watu wa nje ambao huishia kuvuruga uhusiano wa wenzao.
Mfano kama wewe ni mwanamke unayepata kipato kwa kuajiriwa au kwa ujasiriamali, unashindwaje kumtoa out mwenza wako na kusubiri utolewe wewe tu?
Huo siyo usawa hata kidogo, kama hukuwa na utamaduni huo hebu anza ili umfurahishe mumeo tena siku utakayomtoa out muandalie na zawadi kama anavyokufanyia.
Hakikisha siku hiyo bili ya chakula, vinywaji pamoja na malipo ya hoteli kama utaamua kulala na mumeo eneo tofauti unalipa wewe, nakuambia kwa sapraizi utakayomfanyia atakushukuru na kuona ni jinsi gani unamjali.
Nimezungumzia suala la kulala hoteli kwa sababu wanandoa kubadilisha mazingira japo kwa mwezi mara moja siyo mbaya kwani hata kama mumeo ni ‘goigoi’ unaweza kushangaa kwa kulala naye kwenye hoteli ya nyota tano anaweza kuwa vizuri zaidi kisaikolojia kutokana na utulivu utakaokuwepo hotelini na kukupa burudani ya aina yake. Bye!
Note: Only a member of this blog may post a comment.