Imelda Mtema
AIBU! Kisa
utapeli, mrembo Brigita Vitalis, mkazi wa Mtoni Kijichi anasakwa na
polisi kwa RB 20 baada ya kudaiwa kuwaingiza chaka watu 20 ambao
waliungana na kumfungulia mashtaka Kituo cha Polisi Magomeni na kupewa
hati ya mashtaka iliyosomeka; MAG/RB/9768/2015.
Mmoja wa watu waliotapeliwa na mrembo huyo aliyejitambulisha kwa jina la Diana alimueleza kamanda wa Kikosi cha Kufichua Maovu cha OFM kuwa aliingizwa kwenye utapeli na rafiki yake aitwaye Anna ambaye alimwambia kuwa kuna rafiki yake anaitwa Brigita anawatafutia watu kazi lakini ili upate ni lazima utoe pesa. “Kwa sababu ya ugumu wa kupata kazi tulikubaliana na Brigita hivyo tulitoa shilingi laki mbili kila mmoja na kazi hiyo ilikuwa ya Supermarket ya Uchumi,” alisema Diana.
Aidha Diana alisema baada ya kukaa muda mrefu bila kuitwa alifuatilia na ndipo yeye na rafiki yake Anna waligundua kuwa wametapeliwa kwani waliambiwa kuwa Uchumi hawajawahi kuhitaji wafanyakazi wala hawajatangaza, wakaamua kutupia mtandaoni picha ya Brigita na kumtangaza kwa utapeli aliowafanyia kwani alishakusanya pesa za wengi.
“Tulikubaliana kumfungulia mashtaka na moja kwa moja tukaenda Kituo cha Polisi Magomeni ambapo tuliandikiwa hati ya mashtaka iliyojumuisha malalamiko ya watu wote,” alisema Diana.
Baada ya OFM kupata taarifa hizo, walimsaka Brigita kwa mbinu zao na kufanikiwa kumpata ambapo alisema kuwa yeye hakuwa na nia ya kuwatapeli hao watu lakini kuna kijana aliwaambia kuwa kuna kazi Uchumi ndipo alimtaarifu Anna rafiki yake ili awaambie ambao hawana kazi kwani hata yeye alitoa hela yake.
“Hata mimi nilitapeliwa kama wao na aliyefanya yote haya ni kaka mmoja Mkenya hivyo naona waliofikisha habari hii hapa wananifanyia fitna tu,” alisema Brigita pasipo kuelekeza aliko huyo aliyemuita Mkenya.

Note: Only a member of this blog may post a comment.