Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, akionyesha karatasi yenye
orodha ya majina ya wakwepa kodi bandarini, Ikulu jana.
PICHA:
MPIGAPICHA WETU
Kasi
ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kupambana na ubadhirifu wa mali ya
umma, imezidi kupamba moto baada ya Rais Dk. John Magufuli, kumsimamisha
kazi, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade,
kufuatia ziara ya kushtukiza iliyofanywa na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa, jana katika Mamlaka ya Bandari (TPA).
Kufukuzwa kazi kwa Kamishna Mkuu huyo kunafuatia kuthibitishwa kwa
taarifa za kupitishwa kinyemela bandarini hapo makontena 349 na
kuikosesha serikali mapato ya Sh. billioni 80.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa jana Ikulu na Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, nafasi ya Bade inakaimiwa na Katibu
Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk. Phillip Mpango.
Pamoja na kusimamishwa kazi kwa Kamishna mkuu huyo, Balozi Sefue
alisema kuanzia sasa maofisa wote wa TRA hawaruhusiwi kusafiri nje ya
nchi hadi uchunguzi dhidi ya tuhuma mbalimbali zinazo wakabili,
utakapokamilika.
Hatua hiyo ya Rais Magufuli inafuatia ziara ya kushtukiza ya Waziri
Mkuu aliyoifanya jana katika Mamlaka ya Bandari ambapo alizungumza na
viongozi wa mamlaka hiyo na viongozi wa Mamlaka ya Mapato (TRA).
Majaliwa alitangaza kuwasimamisha kazi maofisa watano wa TRA kwa
uzembe uliosababisha kupitishwa kwa makontena 349 na kuisababishia
serikali hasara ya Sh. Billion 80.
Kwenye mazungumzo yao jana asubuhi, Majaliwa alimtaka Kamishna Mkuu
wa TRA, Bade na Naibu Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Lusekelo Mwaseba
kuhakikisha wanashirikiana na polisi kufuatilia upotevu huo na
kuhakikisha fedha hizo zinapatikana na kurudishwa serikalini.
Waziri Mkuu aliwataja baadhi ya maofisa waliosimamishwa kazi kuwa
ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa
Wateja, Habibu Mponezya.
“Hawa wanasimamishwa kazi...IGP ninaagiza hawa watu wakamatwe na
kuisaidia polisi hati zao za kusafiria zishikiliwe na mali zao
zikaguliwe kama zinaendana na utumishi wa umma,” alisema Majaliwa wakati
akimwagiza IGP, Ernerst Mangu ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo.
Majaliwa pia aliwasimamisha kazi Mkuu wa kitengo cha Tehama, Haruni
Mpande, Hamisi Ali Omari (hakutaja ni wa Idara gani) na Mkuu wa Kitengo
cha Bandari Kavu, Eliachi Mrema.
“Hawa wanasimamishwa kazi hadi uchunguzi utakapokamilika na pia
naagiza wakamatwe na wawe chini ya uangalizi wa polisi,” alisema.
Majaliwa pia aliagiza watumishi watatu wa mamlaka hiyo wahamishwe
kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani ambao ni Anangisye Mtafya,
Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimwagiza Katibu Mkuu wa
Hazina, Dk. Servacius Likwelile, ambaye alikuwa kwenye kikao hicho,
kuhakikisha anapeleka wataalamu kutoka Wakala wa Serikali Mtandao
(e-Govt) haraka iwezekanavyo ili wakakague mifumo ya taarifa na kubaini
jinsi ambavyo wizi huo unafanyika.
“Nataka uchunguzi uanze mara moja, tafuteni njia ambazo zinatumika
kama mianya ya wizi kutokea hapa bandarini hadi kwenye bandari
kavu…nataka hayo makontena yatafutwe hadi yajulikane yako wapi na
hakikisheni hizo fedha zilizopotea zinarudi serikalini,” alisema.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini
(IGP), Ernest Mangu, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florens
Turuka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka, Kamanda
wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Bandari (TPA), Awadh Massawe na maofisa mbalimbali kutoka TRA
na TPA.
Akijibu maswali ya Waziri Mkuu, Kamishna Mkuu wa TRA, Bade alikiri
kuwa kuna makontena ambayo yamekuwa yakipitishwa bila kulipiwa ushuru
na kwamba mchezo huo umekuwa ukifanyika kati ya bandarini na bandari
kavu hasa ile iliyoko Ubungo.
BADE ABANWA
Akitoa ufafanuzi, Bade alisema walifanya ukaguzi kwenye bandari
kavu moja moja na kukuta makontena 54 yakiwa yameondolewa kabla ya
kulipiwa ushuru.
“Hata hivyo tulipoendelea na ukaguzi, namba iliongezeka na kufikia
327…..tunaendelea kufuatilia kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupambana na
Kuzuia Rushwa (Takukuru)….mmiliki wa bandari kavu ya Ubungo ametakiwa
kulipa Sh. billioni 12.6 na hadi sasa ameshalipa Sh. billioni 2.4,”
alisema.
Alipoulizwa na Waziri Mkuu kama ana majina ya watumishi
wanaohusika na wizi huo, Bade alikiri kuwa nayo, lakini kwenye mkutano
huo asingeweza kuwa nayo hadi atafutiwe na wasaidizi wake.
Baada ya maelezo hayo, Waziri Mkuu alimuonyesha Kamishna huyo
orodha ya makontena 349 yenye taarifa zote hadi namba za magari
yaliyobeba mizigo hiyo, lakini hayakulipiwa ushuru.
Kamishna Bade alikiri kwamba orodha hiyo iliyoonyeshwa na Waziri
Mkuu kwenye mkutano huo ni ya kweli na ndipo Majaliwa alipokuwa mkali na
kutaja majina ya maofisa wanaosimamishwa.
“Kwa utaratibu huu hatuwezi kufika labda baadhi ya watu waondolewe
kazini, alisema ,” alisema kisha kutaja maofisa watano waliosimamishwa
kazi.
KOVA
Kufuatia agizo la Waziri Mkuu la kuwakamata maafisa wa TRA
waliosimamishwa kazi, Kamanda Kova, alisema mpaka sasa jeshi lake
linawashikilia maofisa wanne na mmoja kati hayo anaendelea kutafutwa.
CHANZO:
NIPASHE
Note: Only a member of this blog may post a comment.