Monday, September 14, 2015

Anonymous

YANGA SC Watamu…Aisee!

IMG_8926Hans Mloli,Dar es Salaam MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga, jana walianza ligi kwa kishindo baada ya kuifumua Coastal Union ya Tanga kwa mabao 2-0, kwenye mchezo mkali uliopigwa katika Uwanja wa Taifa, Dar.
Huu ulikuwa mchezo wa kwanza wa Yanga baada ya ligi hiyo kuanza juzi Jumamosi na hawakufanya makosa baada ya kuibuka na pointi tatu muhimu ambazo ni sahihi mtu akisema ‘Yanga Watamu Aisee’.
Ushindi huu wa kwanza unawafanya Yanga kuanza kwa kukaa kileleni mwa ligi kwa kuwa hadi sasa wenyewe tu ndiyo wamefanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0, huku kila timu ikiwa imeshacheza mchezo mmoja.
Mfungaji bora wa msimu uliopita, Simon Msuva, alianza kwa kasi ya kutetea tuzo yake baada ya kuifungia Yanga bao la kwanza katika dakika ya saba tu ya mchezo akimalizia pasi safi kutoka kwa Amissi Tambwe, ambaye msimu uliopita alishika nafasi ya pili kwa kupachika mabao.
Msuva ambaye kwenye michezo zaidi ya 12 ya kujipima nguvu pamoja na ile ya Kombe la Kagame, alifanikiwa kufunga bao moja tu, jana alionyesha kiwango cha hali ya juu huku akipoteza nafasi kadhaa za wazi.
Katika dakika ya 42 ya mchezo huo, mshambuliaji aliyekuwa anasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa Yanga ili aonyeshe makeke yake, Donald Ngoma, alifanya kazi nzuri baada ya kuifungia timu yake bao safi la pili baada ya kuiwahi pasi safi ya kichwa iliyopigwa na Tambwe ambaye alitoka kipindi cha pili na kuingia Malimi Busungu.
Bao hili la Ngoma ambaye alipiga jumla ya pasi 21, huku tatu tu zikipotea, lilishangiliwa zaidi na mashabiki wa Yanga kwa kuwa walikuwa wanasubiri kwa hamu kubwa kumuona mshambuliaji huyo akitupia mpira kimiani.
“Mchezo ulikuwa mgumu sana, tulipata nafasi nyingi za kufunga lakini tukashindwa kuzitumia, ingawa kupata ushindi wa mabao 2-0 siyo kitu rahisi, naamini wachezaji wangu wamefanya kazi nzuri,” alisema kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm.
IMG_8964Hata hivyo, pamoja na kwamba huu ulikuwa mchezo wa kwanza, Yanga ambao kipa wa zamani wa timu hiyo Manyika Peter alikuwa kwenye benchi kama kocha wa makipa baada ya Juma Pondamali kwenda masomoni, walionekana kuwa kwenye kiwango kizuri zaidi na kuonyesha kuwa ni timu ambayo imekaa pamoja kwa muda mrefu.
Mabeki wa timu hiyo, wakiongozwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, walionekana kuonana vyema huku Thaban Kamusoko, ambaye alicheza kiungo wa kukaba akionyesha kiwango kizuri sana kwa kupiga pasi 58 na kupoteza nne.
Hata alipotoka Mwashiuya na kuingia Deus Kaseke, bado wachezaji wa Yanga walionekana kufanya kazi kubwa sana.
Tambwe pamoja na kwamba hakufunga bao lakini anashikilia rekodi ya mchezaji aliyetoa pasi nyingi za mabao hadi sasa akiwa ameshatoa mbili, huku akiwa amepiga jumla ya pasi sita tu na mbili zikizaa mabao.
Hata hivyo, kuonyesha kuwa mchezo huo ulikuwa na nidhamu ya hali ya juu, ulimalizika bila kadi yoyote.
“Tulishindwa kucheza vizuri kipindi cha kwanza, lakini tuliporejea kipindi cha pili tulicheza vizuri ingawa tulishindwa kutengeneza nafasi nyingi,” alisema Jackson Mayanja, Kocha wa Coastal Union.
Yanga iliwakilishwa na: Ally Mustapha Bathez, Mbuyu Twite, Haji Mwinyi, Cannavaro, Kelvin Yondani, Kamusoko, Msuva, Haruna Niyonzima, Tambwe, Ngoma a Mwashiuya.

Coastal Union: Sebwato Nicholaus, Hamad Juma, Yassin Mustapha, Ernest Joseph, Tumba Sued, Said Jellan, Ali Ahmed Shiboli, Youssouf Sabo na Nassor Kapama.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.