Friday, August 7, 2015

Anonymous

UCHAGUZI MKUU 2015: Mengine ni mbwembwe tu, tunachotaka ni maisha bora!

magufuliDk. John Pombe Magufuli
BAADA ya kusubiri kwa muda mrefu, hatimaye vuguvugu rasmi la uchaguzi mkuu wa mwaka huu limeshika kasi. Tayari Watanzania wenzetu, wameshatangazwa na vyama vyao kuwania nafasi ya urais huku kura za maoni kwenye udiwani na ubunge zikiendelea nchi nzima. 

Wapo watu wanabeza wagombea wa vyama vingine, kwa sababu wao wanaamini mvutano mkubwa utakuwa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) unaoundwa na muungano wa vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD. 

CCM itawakilishwa na mgombea wake Dk. John Pombe Magufuli huku Ukawa wakiwa na Edward Ngoyai Lowassa, wanasiasa ambao hadi mwanzoni mwa mwezi uliopita walikuwa ni makada wa chama kimoja. 

Wengine waliochukua fomu za kuwania urais kutoka Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) ni Hashim Rungwe wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chausta), Christopher Mtikila wa DP na Fahmi Dovutwa kutoka United Peoples Democratic Party (UPDP).
10.Lowassa akizungumza jambo.Edward Ngoyai Lowassa
Waswahili wana msemo kuwa mdharau mwiba mguu huota tende, wakimaanisha kuwa kile kitu ambacho mtu anakiona kidogo, kisicho na maana, ipo siku anaweza kujikuta akipatwa na mshangao kwa kitakachotokea.

Maana yangu ni kuwa ingawa wagombea hawa wawili, Magufuli na Lowassa wanapewa nafasi kubwa ya mmoja wao kuibuka kidedea, wito wangu kwa wananchi wote, kuwa makini sana na wanadi sera wote wanaowania kuwa viongozi wetu, iwe katika nafasi hiyo kubwa kabisa, au hata ubunge na udiwani.

Sarakasi zimekuwa ni nyingi sana huku mbwembwe zikitawala kila kona ya nchi lakini kikubwa ambacho wananchi wanakipenda kitokee ni kuboreshwa maisha yao. Katika hili, wakati mwingine chama siyo kitu cha msingi sana, isipokuwa mtu mwenyewe anapaswa kupewa kipaumbele.
Christopher-MtikilaChristopher Mtikila
Ni hadi pale tutakapochukua muda na kuwasikiliza wanachokisema kwenye majukwaa, ndipo tunapoweza kuwa na chaguo bora, linaloweza kuaminiwa kwa ajili ya ustawi wa maisha yetu mmojammoja, lakini pia kama taifa.
DSC_7629Fahmi Dovutwa
Tunapokwenda kwenye mikutano ya hadhara ya kisiasa, tusitazame sura ya mtu wala mbwembwe zinazoendana na mkutano anaohutubia, bali tuwe makini kumsikiliza mgombea, kwa sababu licha ya kuwa kila mmoja ataongozwa na ilani ya chama chake, lakini yapo mambo mengine ambayo yanamtegemea mgombea mwenyewe binafsi.

Kuna watu miongoni mwa wagombea wetu, wanafahamika kutokana na utendaji wao wa kazi, dhamira zao katika kuwaongoza wenzao na hata uwajibikaji wao. Huu ni wakati wa kuwatafuta na kuwasikiliza vizuri mikakati yao, ili siku ya kupiga kura itakapofika, tusiwe tena na kujiuliza juu ya chaguo letu.

Kama hatutajenga utamaduni wa kwenda kuwasikiliza wagombea katika majukwaa yao ya siasa, hakika hatuwezi kuwapata wagombea bora wa kuondoa matatizo yetu. Kama sisi tutawasubiri wenzetu watuhadithie habari za wanasiasa tukiwa baa, sokoni au kwenye maeneo yetu ya kazi, ni vyema tukaelewa kuwa wasimuliaji hawatatueleza kilichosemwa mkutanoni, bali alichokielewa yeye.

Na ubaya wa kusimuliwa ni kuwa msimuliaji atamvutia msikilizaji kuwa upande wake, hivyo kukuondolea haki yako ya msingi ya kuamua bila shuruti.

Huhitaji mikutano kumi kumsikiliza mtu mmoja ndipo upate kumwelewa. Mtu mwenye dhamira ya dhati huonekana hata kwa kumtazama tu, hivyo mkutano mmoja au miwili ya kumsikiliza mgombea inatosha kumfanyia tathmini.

Baada ya kumsikiliza, sasa utakuwa na nafasi kubwa ya kujadili kuhusu wagombea ukiwa na wenzako, na hivyo mwisho wa siku kujiridhisha kuwa huyu ndiye chaguo lako sahihi kwa msimu wa miaka mitano ijayo.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.