Friday, August 28, 2015

Anonymous

MKWASA: Hatujaja Uturuki Kuangalia Maghorofa!

Mkwasa-Stars

Saleh Ally, Kartepe
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa, amesema hawapo hapa kwa ajili ya kuangalia ubora wa maghorofa katika nchi hii ya Uturuki, badala yake ni kazi kuhakikisha Nigeria wanapigwa hiyo Septemba 5, mwaka huu.
Stars imeweka kambi kwenye mji huu wa Kartepe nchini Uturuki kujiandaa na mechi hiyo dhidi ya Nigeria kuwania kucheza Afcon. 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mkwasa amesema maandalizi yanakwenda vizuri na pamoja wamejikita vilivyo kwenye kuhakikisha ushindi unapatikana.
“Kweli, tuko makini sana kama ambavyo umeona na tumekuwa tukijituma sana kuhakikisha kila kitu kinafanikiwa. Wachezaji wote wako fiti kama unavyoona, kasoro Banda tu ambaye ameumia, lakini mambo yanakwenda vizuri na kazi inafanyika,” alisema. 

Jana, Stars ilifanya mazoezi mara moja tu kwa kuwa leo ina mechi ya mazoezi dhidi ya timu ya taifa ya Libya. Awali, Stars ilikuwa icheze mechi ya kirafiki dhidi ya Iraq, baadaye ikagundulika haikuwa timu ya taifa badala yake ni klabu, hivyo ikaahirishwa. 

Baada ya mechi ya leo, Stars haitakuwa na mechi nyingine na Mkwasa amesema wataanza kufanya marekebisho kadhaa.
“Tutaanza kurekebisha yale ambayo tutayaona katika hiyo mechi mazoezi. Maana tutacheza kwa lengo la kujiweka vizuri na mechi hiyo si ya mashindano au kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa. Ndiyo maana tutaangalia zaidi kujifunza kuliko ushindi,” alisisitiza Mkwasa.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.