Sunday, August 16, 2015

Anonymous

MBUNGE WA MBINGA ANYANGANYA VIPAZA SAUTI BAADA YA KUSHINDWA UCHAGUZI

ALIYEKUWA mbunge wa Jimbo la Mbinga Mashariki Gaudence Kayombo, ambaye aliingia katika mchakato wa kura za maoni jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amewashangaza wanachama wa chama hicho baada ya mbunge huyo kwenda ofisi za CCM wilayani humo kunyang’anya vifaa vya matangazo, ambavyo ni vipaza sauti baada ya kushindwa kwenye mchakato wa uchaguzi wa kura za maoni uliofanyika Agosti Mosi mwaka huu.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti mjini hapa, wanachama hao walisema kuwa Kayombo alifanya hivyo baada ya kuwasili katika ofisi hizo za chama Agosti 14 mwaka huu majira ya asubuhi, akionekana mtu mwenye hasira.

“Huyu Mbunge alipowasili pale ofisi za chama alitushangaza sana, alikuwa mtu mwenye hasira huku akizungumza kwa ukali anataka vifaa vyake vya matangazo ambavyo alikinunulia chama, huku akitamka maneno kwamba ameamua kufanya hivyo kwa sababu viongozi wa chama wilaya hawamtaki”, walisema.

Aidha walifafanua kuwa kitendo alichofanya Kayombo ni cha aibu, kwani yeye akiwa mwanachama wa CCM anapaswa kuendelea kukisaidia chama kwa mambo mbalimbali na sio kufanya kitendo kama hicho, cha kunyang’anya vitu ambavyo alikipatia chama.

Walibainisha kuwa Mbunge huyo baada ya kuona ameangukia pua kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni zilizofanyika hivi karibuni, muda mwingi alikuwa akiwalaumu viongozi wa chama hicho wilaya ya Mbinga akisema kuwa ndiyo waliochangia aweze kudondoka katika mchakato huo.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Mbinga, Zainabu Chinowa alithibitisha hilo na kueleza kuwa wao kama chama wamesikitishwa na kitendo hicho ambacho hawakutegemea Kayombo kama angeweza kufanya hivyo.

“Huyu mtu ametushangaza sana, hili jambo alilofanya ni aibu yake yeye mwenyewe tunajua kitendo hiki cha kutunyang’anya vipaza sauti ni hasira zake alizonazo baada ya kushindwa, kwenye uchaguzi wa kura za maoni”, alisema Chinowa.

Gazeti hili lilipomtafuta Kayombo kwa njia ya simu, ili aweze kuzungumzia hilo hakuweza kupatikana kutokana na simu yake kuita kwa muda mrefu, bila kupokelewa.

Kwa upande wake katibu wa CCM wa mkoa wa Ruvuma Vellena Shumbusho akizungumza na nipashe jana ofisin kwake alisema kuwa amelazimika kumwagiza katibu wa CCM wa mbinga Chinowa kumkabithi haraka sana vifaa anavyodai Kayombo alivyokuwa amevinunua na kukabithi kwenye chama kwa ajili ya kusaidia matangazo wakati wa machakato wa kura za maoni

Hata hivyo CCM kwa upande wa jimbo la Mbinga vijijini kulikuwa na wagombea ubunge nane ambao waliingia kwenye mchakato huo wa kura za maoni uliofanyika Agosti Mosi mwaka huu ambao ni; Martin Msuha aliyeongoza kwa kupata kura (13,354), Gaudence Kayombo (12,068), Humprey Kisika (545), Dokta Silverius Komba (3,941) na Deodatus Ndunguru (7,060) matokeo hayo yalitangazwa Agosti 3 mwaka huu majira ya saa 5:45 usiku na Katibu wa Chama hicho wilaya ya Mbinga, Zainabu Chinowa.
MWISHO.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.