Mawaziri wawili wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete
wameanguka kwenye marudio ya Kura za Maoni zilizofanyika juzi, huku
matokeo ya Jimbo la Busega yakikwama baada ya Waziri wa Uvuvi na
Maendeleo ya Mifugo, Dk. Titus Kamani kumshambulia msimamizi wa Uchaguzi.
Walioanguka ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid (Rufiji) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mazingira), Dk. Binilith Mahenge (Makete), huku Dk Raphael Chegeni akiongoza kwenye Jimbo la Busega.
Dk Kamani na wafuasi
walizuia matokeo kutangazwa na kuibuka kwa vurugu zilizosababisha polisi
kuingilia kati na kukamata watu wanne walioonekana kumuunga mkono.
“Aliyeshinda
ameshinda tu hakuna namna. Kilichofanywa na Waziri Kamani kumpiga
msimamizi huyo ni mambo ya binadamu tu… lakini walioshindwa lazima
wakubali matokeo na lazima yatangazwe,” alisema Paul Mzindakaya, Mkuu wa Wilaya ya Busega.
Vurugu zilianza saa 4 asubuhi baada ya
Dk Kamani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Simiyu, kuingilia
kati wakati Mabiya, ambaye ni katibu wa Wilaya ya Meatu, akianza
kutangaza matokeo.
Baada ya Polisi waliokuwa na silaha
kuimarisha ulinzi, Mabiya alisimama kutangaza matokeo lakini akakatishwa
baada ya kurukiwa na watu walioonekana kumuunga mkono Waziri Kamani na kupigwa makonde mbele ya Polisi na Mzindakaya.
Kipigo hicho kilimfanya Mabiya akimbilie ndani ya ofisi za chama hicho na kuacha askari wa Kikosi cha FFU wakitumia nguvu kudhibiti watu hao.
Wakati wote wa vurugu hizo, Dk. Chegeni
alikuwa amesimama pembeni mwa ofisi za chama hicho akishuhudia matukio
hayo, lakini baadaye akaondoka akiwa amepanda gari lake huku
akishangiliwa.
Baada ya polisi kufanikiwa kutuliza
ghasia, Mabiya alisimama tena kutangaza matokeo hayo, lakini Dk Kamani
alimfuata na kumshambulia kwa makonde, kukazuka tafrani kubwa zaidi.
Note: Only a member of this blog may post a comment.