Wednesday, August 12, 2015

Anonymous

HONGERA GENIUS NIKKI, MUZIKI UNAHITAJI VICHWA KAMA WEWE!

KWAKO Nickson Simon ‘Nikki wa Pili’ mambo niaje? Uko poa? Za tangu wiki iliyopita tulipoonana kwenye tafrija ya kumuaga Rais Jakaya Kikwete?
Ukitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima. Niko poa, naendelea na mishemishe zangu kama kawaida. Miongoni mwa majukumu yangu ni hili la kuwaandikia nyinyi mastaa barua, kuwapongeza au kuwakosoa pale mnapotoka nje ya mstari.

Dhumuni la kukukumbuka leo kwa barua hii ni kutaka kukupongeza. Nakupongeza maana umeonesha unajua nini unatakiwa kufanya kama msanii. Tena si tu msanii, msanii msomi unayejitambua.

Kupitia hotuba yako uliyoitoa siku ile katika hafla ya kumuaga Kikwete, kwa kujiamini ulieleza namna ambavyo umekuwa bega kwa bega kushirikiana na serikali kuhakikisha sanaa inakuwa sekta rasmi. Itambulike, ichangie pato la taifa kwa maana ya kodi.

Ulieleza namna ambavyo umeshirikiana na serikali kufanya tafiti mbalimbali ambazo zimeleta majibu chanya katika sanaa. Ni jambo jema sana. Nakupongeza pia kwani ulikuwa miongoni mwa wasanii waliopigania suala la miito ya simu (ring tone).

Wasanii kutolipwa vizuri na makampuni ya simu katika huduma ya ring tone, ni tatizo kubwa. Wasanii wengi walikuwa wakilalamikia chinichini, hawakufikisha katika mamlaka husika. Wewe uliweza kutumia fursa, ukajitoa wakati mwingine kutumia hadi muda wako binafsi kufanikisha mambo ya jumuia.

Angalau ulisema mmefikia hatua ya kuanza kulipwa vizuri. Jitihada zako na watu wanaokuzunguka, zimekuwezesha kumfikia rais Kikwete. Kiongozi mkubwa wa nchi, si kazi ndogo.Uliweza kuwasiliana naye mara kwa mara, kumueleza maendeleo ya ‘projekti’ mbalimbali mlizokuwa mmekubaliana.

Umepigania suala la ‘stika’ katika kazi za wasanii. Umeonesha mfano. Kupitia hotuba yako, ulionesha namna ambavyo umefanya kazi kisayansi. Kwa kuangalia nchi za wenzetu wanafanyaje ili kukomesha maharamia.
Nawajua wasanii wetu walivyo wazito hata katika kufanya mambo yao ya msingi. Ushahidi ni kile kikao cha wasanii kilichowahusisha nyinyi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hivi karibuni. Wenzako wengi hawakutokea lakini wewe ulitambua umuhimu, ukaenda na kushiriki.

Huo ni mfano mdogo tu. Tasnia hii inahitaji mtu kama wewe, utakayesimama kidete kutetea na kuieleza serikali, naiona kesho yako ilivyo njema. Uzuri unaendelea na masomo, elimu yako itakuwa na manufaa makubwa sana huko mbeleni.

Nikusihi, endelea kuikaba koo serikali kama ulivyosema katika hotuba yako. Kwamba rais ajaye naye ana kazi kubwa ya kuendeleza pale alipoishia rais Jakaya.Nikutakie kazi njema, Mungu azidi kukubariki, endelea kutetea maslahi yenu!
Ni mimi, Erick Evarist

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.