Wednesday, August 12, 2015

Anonymous

HATARI SANA! Haya mabasi ya Mikoani, wee acha tu!

9.TaswilanzimayamabasiyaendayoMikoanikatikastendiyaUbungo.
Niliamka saa kumi alfajiri ili niweze kuwahi basi la kwanza ili nifanye safari yangu ya mkoa. Nilimpigia simu Bodaboda, akaja huku akilalamika kuwa nimemuamsha mapema mno, hatimae nikajikuta ndani ya basi nikiwa nimekaa kwenye kiti nilichopangiwa.

Sikukaa muda mrefu akaingia mama mmoja naye akakaa pembeni yangu, tukasalimana vizuri na kutulia kungoja safari ianze. Basi likajaa saa kumi na mbili safari ikaanza, haikuchukua muda usingizi ukanichukua, maana jana nilichelewa kulala kwani kulikuwa na shughuli nyingi za kifamilia na kama nilivyosema niliwahi sana kuamka ili niwahi usafiri.

Nilishituliwa na sauti kali ikitangaza, “Samahani wasafiri, samahani kwa usumbufu’ kumbe alikuwa ni yule mama aliyekuwa kakaa pembeni yangu, kwa muda nikashangaa kuna nini? Au kaibiwa? Bila kungoja jibu kama amesamehewa au la, yule mama akaanza matangazo.

“Naitwa Mama Fule, hapa nauza vitu mbalimbali, krimu hii hapa inaondoa chunusi, na inamsaidia mtu mwenye ngozi nyeusi sana kuwa nyeupe kidogo, krimu hii ni nzuri sana kwa wenye magaga, ukitumia wiki mbili miguu inakuwa kama ya mtoto mchanga, na hii hapa ni dawa ya mswaki nzuri sana, ukitumia hii meno yaliyooza yatapona na inasaidia wale wavuta sigara kuacha kuvuta.”

Nikasikia miguno ya wenzangu waliokuwa wanasumbuliwa kama mimi na mjasiriamali huyu. Wala hakuonesha kujali kuwa anasumbua watu akaendelea. “Hapa nina sabuni ya kuoshea nywele, inasaidia hata kama una kipara kinaota nywele, pia nauza vitabu vya watoto, hivi vinasaidia watoto kujifunza kusoma’ Wakati anaendelea na kelele zake nikajiuliza hivi hakuna sheria ya kuwadhibiti hawa watu?

Nilitegemea kupumzika baada ya kuwahi kuamka, huyu mama anahakikisha ananitangazia bidhaa ambazo sina haja nazo na sina la kufanya. Hatimae akanyamaza na kuanza kuzungusha biashara yake kwa wateja katika basi. Wakati namshukuru Mungu kwa ukimya nikaanza kupata tena usingizi. Ghafla nikasikia tena, ‘Samahani wapendwa katika Bwana’ , safari hii alikuwa mwanaume aliyevaa suti na tai nzuri, wakati nawaza huyu naye anauza nini? Jamaa akaanza mada yake moja kwa moja. “Wapendwa je, ni wangapi wanataka kwenda mbinguni? Kuna watu mambo wayafanyayo ni wazi hawawezi kwenda mbinguni, leo nimeona niwaoneshe njia ya kwenda mbinguni, najua wengine mmelala, amkeni msikie neno litakalowaokoa, amkeni amkeni amkeni wapendwa.”

Wala hakufika mbali zogo likaanza ndani ya basi, wengine wakipiga kelele kuwa wako madhehebu tofauti, hawahitaji mahubiri hayo wengine wakimuunga mkono mzee mwenye suti aendelee, wengine tukilalamika kuwa tunasumbuliwa tumechoka na hatutaki kuamka, kidogo ngumi ziumuke basi likiwa katika mwendo mkali, kila aina ya sauti ilisikika, mwenye suti akiendelea na mahubiri yake kwa nguvu, jamaa mmoja nikamsikia akimpigia kelele dreva awashe muziki, huku kundi moja likimhamasisha mwenye suti aendelee, wenye madhehebu tofauti wakilalamika kwa nini wanalazimishwa kusikiliza kisicho wahusu, jamaa wawili tayari walishafikia hatua ya kutishiana kutandikana ngumi, usingizi wote ulikuwa umenikimbia, nikawa nawaza kwa nini mtindo huu wa kulazimishwa kusikiliza kisichokuhusu unaendelea katika mabasi?

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.