Wednesday, July 29, 2015

Anonymous

HUJAFA HUJAUMBIKA! MATESO ANAYOPATA KIJANA HUYU USIOMBE YAKUKUTE!

Na Imelda Mtema
Kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Noeli Lazaro (26), mkazi wa Mtwara, kitongoji cha Mangamba, yuko katika mateso makali baada ya kupata ajali akiwa anaendasha Bajaj.

Ajali hiyo imemsababishia kuvunjika mgongo wake hivyo kushindwa kusimama wala kutembea.

Akizungumza akiwa katika mateso makali Noeli anasema:
“Nakumbuka siku hiyo ilikuwa majira ya saa mbili usiku nikiwa na abiria wangu mmoja, kuna mtu ambaye sikuweza kumfahamu alikuwa akiniwashia taa za gari lake kwa kuzichezesha akiwa barabarani mjini Mtwara.

“Baada ya mtu huyo kufanya hivyo, sikuweza kujizuia hivyo nikaingia kwenye mtaro mkubwa na hapohapo nikapoteza fahamu na hata gari la polisi lilipokuja kunichukua, nilikuwa sijijui.
“Nilizinduka nikiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Ligula, mkoani Mtwara ambapo waliponipiga x-ray waligundua kuwa pingili zangu za mgongoni zimepishana.

“Waliniambia zinahitajika shilingi laki nne kwa ajili ya kunisafirisha kwa gari la hospitali hadi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi, sikuwa na fedha hizo.
“Nilikata tamaa ya maisha lakini kwa bahati nzuri hospitali walijitolea wakalipia fedha hizo nikasafirishwa hadi hapa Muhimbili, naushukuru sana uongozi wa Hospitali ya Ligula.”

KUWEKEWA VYUMA
“Muhimbili nilipopimwa na kugundua mgongo umevunjika walinifanyia upasuaji na kuniwekea vyuma.

“Baada ya matibabu hayo niliruhusiwa kurudi Mtwara, ilikuwa kazi kubwa kwa sababu sikuwa na fedha. Hata hivyo, nilifanikiwa kupata nauli nikapanda basi kurejea nyumbani.

VIDONDA VYAFUMUKA
“Nilifika Mtwara nikapata matatizo mengine kwani safari hiyo ndefu ilisababisha nyuzi nilizoshonwa kuachia, kidonda kikafumuka.

Kutokana na tatizo hilo, nikaenda Hospitali ya Ligula ambapo nililazwa kwa ajili ya kuuguza kidonda.
“Niliruhusiwa kutoka baada ya kidonda kuonesha dalili za kupona lakini nikawa natakiwa kuripoti kliniki ya Muhimbili, nashindwa kwa sababu sina uwezo kifedha kwa ajili ya kutoka Mtwara hadi Dar.

“Mpaka sasa niko katika wakati mgumu sana siwezi kukaa, kusimama, kutembea na maisha yangu ni magumu sana. Naomba msaada kwa Watanzania wenzangu ili niweze kwenda kliniki Muhimbili ili madaktari waangalie maendeleo ya mgongo wangu, vinginevyo nitaishia kuteseka,” alisema Lazaro kwa njia ya simu akiwa Mtwara.
Yeyote aliyeguswa na habari hii awasiliane na Lazaro kwa namba 0685 950 396.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.