Saturday, June 27, 2015

Anonymous

YANGA SC Full Mziki!

Wilbert Molandi, Dar es Salaam
YANGA leo inacheza mechi maalum ya kirafiki na SC Villa ya Uganda kwenye Uwanja wa Taifa, lakini ishu kwao ni kuwasili kwa yule straika miraba minne, Donald Ngoma kuichezea timu hiyo.

Ngoma anatarajia kutua nchini leo Jumamosi kujiunga na kikosi cha Yanga pia wachezaji wawili kutoka Ghana wanatarajiwa kuwasili kuiongezea nguvu timu hiyo na kukamilisha orodha ya wachezaji saba wa kigeni.

Straika huyo raia wa Zimbabwe anayechezea klabu ya FC Platinum, anawasili nchini baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuruhusu matumizi ya wachezaji saba wa kigeni katika timu za Ligi Kuu Bara.

Ukiachana na wachezaji hao waliopangwa kuwasili leo, Yanga pia imeachana na kipa Benedict Tinoco na kumsajili Mudathir Khamis kutoka Zanzibar Heroes anayechezea KMKM.

Hao wanaungana na wageni wengine ambao ni Malimi Busungu aliyetokea JKT Mgambo, Deus Kaseke (Mbeya City) na Hajji Mwinyi kutoka KMKM.

Yanga tayari inao wachezaji watano wa kigeni ambao ni Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite wa Rwanda, Amissi Tambwe (Burundi), Kpah Sherman (Liberia) na Andrey Coutinho wa Brazil.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema, ujio wa Ngoma na Waghana wawili ambao ni kiungo na straika, utafanya kuwe na wachezaji nane, hivyo mmoja kati ya Sherman au Coutinho ataachwa.

Akizungumzia mchezo wa leo dhidi ya Villa, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, aliliambia Championi Jumamosi: “Sasa tupo full, maana kwa mazoezi haya ya wiki mbili tupo katika nafasi nzuri ya kupambana na Villa kesho (leo), hivyo mashabiki wa Yanga waje kuiona timu yao.”

Mchezo huo ulioandaliwa na Nyumbani Kwanza Media Group, umelenga kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi ‘Albino’.

Yanga itatumia wachezaji wake wote hata wale waliopo kwenye kikosi cha Taifa Stars kwani jana usiku walitarajiwa kujiunga na kambi ya timu yao tayari kwa mchezo huo.

Kocha wa Villa, Killya Ibrahim ambaye amepanga kumtumia Lansana Kamara aliyenyimwa usajili na Yanga, alisema: “Tunaijua na kuiheshimu Yanga lakini tumetoka Uganda kuja kupambana.”

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.