Tuesday, June 16, 2015

Anonymous

WEMA SEPETU JITAMBUE...TUPIGE HELA!

Kwanza mambo vipi! Natumaini unaendelea vizuri na maisha yako kama kawaida, tumshukuru Mungu kwani bila yeye, nadhani tusingekuwa mahali hapa wakati huu.
Wema, nimekaa na kujifikiria sana juu ya hili ninalokwenda kuandika, labda ni wivu wa maendeleo ndiyo ulionisukuma kutumia dakika zangu kumi kuandika maneno haya mazito ambayo huku kwetu uswahilini tunayaita nondo.


Nakiri kwamba hakuna mtu ambaye anaweza kufanya biashara ndogo au kubwa na akafanikiwa kwa kiwango kikubwa kama wewe. Umetokea kupendwa mno, umetokea kuwa na mvuto sana, kuna watu wengi wanakupenda na wakiulizwa wanakupendea nini, nao hawajui, ila wanakupenda.

Ninapokuangalia wewe, simuoni Wema, namuona mwanamke fulani masikini, aliyekaa barabarani akiomba fedha, anaonekana kuchoka lakini cha kushangaza, amebeba mkoba wenye kipande kikubwa cha almasi yenye ukubwa kama ngumi.

Wema, nikwambie ukweli tu, unapotembea, jua ni hela ndiyo inatembea,
unapopumua jua ni hela ndiyo inayopumua. Tatizo kubwa kwako linawakumba watu wengi tu nchini Tanzania, hawana washauri wazuri katika maisha yao.


Kabla ya kuongea kile ninachotaka nikiseme, kuna mtu katika maisha ya wengi anaitwa Meneja, huyu kazi yake ni kuangalia wapi hakujakaa sawa, yeye apaweke sawa, si ndiyo? Sasa Wema una meneja wako, tena yupo beneti na wewe kabisa, lakini amekwishawahi kukwambia kwamba wewe ni fedha? Amekwishawahi kukwambia vitu vya kufanya ili uweze kupiga fedha na kuachana na mambo fulanifulani?

Kuna watu wanajiita Team Wema, najua unawajua hawa, wapo tayari kupigwa, kufa, kushambuliwa kwa ajili ya kulitetea jina lako tu. Mtu hajawahi hata kukutana nawe ana kwa ana ila ukichokonolewa tu, wanakuja juu kama moto wa kifuu.
Wema, hawa ni watu wako, hawa ni watu ambao wanaweza kukupa fedha kila siku, tatizo nini? Haujajitambua kama wewe ni fedha mpaka mtu aje akushtue?


Kwa hadhi uliyokuwa nayo, nilitegemea kwamba unaweza kuanzisha hata nguo za ndani kisha zikaandikwa team Wema, hizo tu halafu ukaziuza mtaani, hivi unajua ungeingiza kiasi gani kwa biashara hiyo tu? 

Dada zetu wa mitaani wanaojua biashara wanatamani kuwa wewe, wanatamani wapate jina kama wewe, kuna wengine wanatoa mpaka miili yao ili mradi tu mwisho wa siku waje kuwa kama wewe, ila bahati mbaya, nyota yako imekuwa kali kuliko wengine.
Mtazame msichana kama Jokate, ana jina dogo mno, lakini kwenye jina lake hilohilo, kajipinda na kuanzisha viatu vyake vya kike na kuvipa jina la Kidoti, anapiga hela na watu wamekuja kuwekeza, sasa wewe unashindwa nini? Hivi kweli kama Jokate anapiga hela na kuingia mkataba wa mamilioni ya shilingi, vipi kuhusu wewe?
Umri unakwenda Wema, hizi team zinazoonekana si za kuziamini tena, kuna siku msichana fulani ataibuka, atakuwa na jina kubwa na kuzima nyota yako, hapo ndipo utakaposhtuka kwamba kuna mambo mengi hujayafanya.


Mtazame mwanamuziki kama Jeniffer Lopez, alipoona amepata jina, akaanzisha mavazi yake na kutaita JLO, katika hayo kulikuwa na sidiria, nguo za ndani na suruali za kike, mwisho wa siku zikamtengenezea fedha sana na kumuinua, vipi kuhusu wewe? Umeshafikiria jambo hilo au bado tunakula bata kwanza?

Una meneja lakini mpaka sasa hivi sijaona kazi yake, nilidhani yeye ndiye angekuwa mstari wa kwanza kukwambia kwamba wewe ni almasi kubwa mno, nilitegemea kwamba yeye ndiye atakuwa wa kwanza kukwambia kwamba huu ni muda wa kutengeneza sidiria zenye jina lako, kumbe, nilichokiona mimi, huyu ni meneja wa maneno, meneja asiyekuwa na ushauri wa maana, sasa kwa nini kuwa naye?

Kinachoniuma, leo hii watu wanaanzisha party zao na kisha kuambatanisha jina lako, wanasema kwamba wewe utakuwepo, wanaingiza fedha sana kwa sababu tu Wema yupo, ukumbi unajaa lakini mwisho wa siku, wanachukua chao na kuondoka zao.
Wema, unatumiwa na wajanja wa mjini, watu wanatengeneza fedha kupitia wewe, hivi kweli hauwezi kusimama wewe kama wewe na ukatengeneza fedha? Huwezi kusema kwamba unaanzisha Wema Party, kiingilio elfu kumi na kila atakayeingia utakuwa ukipiga naye picha? Hivi unahisi utaingiza kiasi gani? 


Jina lako ni biashara sana, nyota kali ya kupendwa uiliyokuwa nayo wewe kama angekuwa nayo Jokate, sasa hivi ni bilionea. Mwisho wa siku, cha kushtua, nasoma magazetini kwamba unagombania bwana na Linah! Kweli wewe, na jina lako kubwa bado unaishi katika ulimwengu huo? Siamini, na kama ninalazimishwa kuamini basi utakuwa unalitumia vibaya jina lako.

Wema, hebu shtuka kwanza, shtuka tupige hela, hebu tambua kwamba jina lako ni fedha. Kim Kardashian anapiga hela kwa kuwa anajua kwamba yeye ni hela, hatumiwi na watu eti kwa kisingizio cha kuanzisha shoo na watu kupiga hela.
Kama akili yako ikifunguka kibiashara na kujitambua wewe ni nani, nakuahidi utakwenda kuwa bilionea. Kampani uliyokuwa nayo haina maana, achana nayo. 


Una kampani hiyo miaka mingi, hawakushauri ulitumie vipi jina lako kupiga hela, wao kutwa nzima kukwambia tukanywe wapi, iache hiyo kampani na utafute nyingine, kampani ambayo itaweza kukwambia kuanzisha biashara ya nguo za ndani, viatu vyenye jina lako, ila hii iliyokuwepo kwa ajili ya starehe, achana nayo kabisa.

Ninachoamini kuna mabilionea ambao fedha zao zinawawasha, wanatamani wasikie ukianzisha biashara ili waje kuwekeza na kukupa mabilioni ya fedha, ila kila wakisubiri, hawaoni kitu hicho zaidi ya kusikia leo Wema kampa makavu Kajala na vitu vingine ambavyo havikuingizii fedha zozote ile.

Wazungu wanasema Time will tell yaani Muda utaongea tu, wakati utakapokuwa umeanza kufifia, muda nao utakwambia hakuna kusubiri zaidi ya kusonga mbele. Kuna mwanamuziki anaitwa Jay Z, alitamka wazi kwamba yeye si mfanyabiashara bali yeye ni biashara, unajua alimaanisha nini?

Maana yake ni kwamba anaweza kupata fedha kupitia jina lake na si yeye ahangaike tena, akatengeneza vitu vingi mno, kweli aliangiza fedha. Unamkumbuka P Diddy kipindi kile alichokuwa akiitwa Puffy Daddy? Alitengeneza nguo zake baada ya kugundua kwamba hata yeye ni biashara na akaziita Sean John, alitengeneza sana fedha, na kweli akawa bilionea.

Wema unashindwa nini? Kuna wanawake kama milioni tatu Tanzania wapo nyuma yako, ukiwaambia twendeni huku, wanafuata, ukiwaambia fanyeni hivi, wanafanya. Umekuwa na nguvu kubwa ya ushawishi, mwaka jana ulimpigia sana promo Diamond kuchukua tuzo, kweli akabeba, mwaka huu ukamtangaza sana Kiba, kweli akabeba, hivi mpaka hapo haujajigundua ni nguvu ya namna gani uliyokuwa nayo?

Sawa, inawezekana kusoma haujui, lakini hata picha hujaiona? Unataka mpaka Mungu akutokee na kukwambia kwamba amekupa nyota kubwa ing’aayo kwa kuwa anataka upige hela? Au kwa sababu wewe si Mchagga hivyo hauna utaalamu mkubwa kuhusu masuala ya fedha?

Wema, mwili wako una thamani zaidi ya bilioni hamsini, lakini unaweza kukuta kwenye akaunti hata bilioni moja hauna, hii inauma sana, inaniuma ninapowaona wanawake wengine wanajishughulisha kufanya biashara, zinakataa, halafu wewe mwenye uwezo wa kupiga hela, wala huna habari, matokeo yao wanakuja wajanja wa town, wanasema kwamba wanaanzisha party, Wema Sepetu a.k.a Madam atakuwepo, ukumbi unajaa, wanachukua manoti yao, wanasema na kukucha solemba, kesho tunaanza kusema kwamba ukumbi ulijaa sana, je pamoja na kujaa huko ulipata nini wewe ambaye jina lako lilitumiwa kuingiza watu wengi?

Wema, una uwezo wa kutengeneza kitabu cha maisha yako, ukatoa kitabu, kikapigiwa sana promo, tena siyo ya vyombo vya habari, hata kurasa zako zinaweza kutumia kukipigia promo huku ukiuza kila kopi elfu kumi tu, hivi ushajifikiria utaingiza kiasi gani?

Ushajua kwamba kwa kopi laki moja tu ambazo naamini zinaweza kuuzwa kwa siku ya kwanza tu kitakuingizia shilingi milioni mia moja. Hivi kweli hizi team Wema haziwezi kumaliza vitabu milioni moja? Ninachokijua si team Wema tu watakaonunua, kila mmoja angependa awe nacho aone ulipopitia, kwa hiyo hata kopi milioni moja, nina uhakika utauza tu kutokana na jina lako. Kwa maana hiyo hivyo vitabu milioni moja vikiisha, tayari mfukoni imeingia bilioni moja, unataka nini tena? Hata Mungu atafurahia kwa kuwa amekupa nyota na umeitumia ipasavyo.

Leo hii, eti Nyemo ndiyo nimegundua vitu ambavyo meneja wako ambaye ni mtu wa karibu hajavigundua, kweli huyo anastahili kuwa meneja, nahisi hastahili kwa kuwa hafanyi kazi zinazotakiwa kufanywa kama meneja.

Wema, kila ukifanyacho, jua hakuna kinachodumu milele, jua kuna siku tutasema kulikuwa na msichana alivuma sana, aliitwa Wema, alikuwa balaa.

Hivi leo ukiambiwa kwamba kulikuwa na mwanamke mwenye jina kubwa kama Jeniffer Lopez ambaye alitamba dunia nzima, utaamini? Je Madonna? Wenzako walizitumia nafasi mara baada ya kuona wamepata jina, sasa kwa nini na wewe usitumie nafasi hizi?

Achana na mabifu na watu wengine, jua mambo yako kwa sasa, piga hela kwani mabifu hayatoweza kukuingizia hela hata siku moja zaidi ya kukupa stress na kukupotezea muda tu. Jitengenezee vipato, kwa jina lako, naamini utaweza tu, kama aliweza Jokate, mwenye jina dogo, utashindwa wewe? Hapana, Wema, huu ndiyo wakati, usisubiri mpaka kengele igonge.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.