Mamlaka ya mawasiliano nchini, TCRA, makampuni ya simu na mamlaka ya
vitambulisho, NIDA, imezindua zoezi la usajili wa simu kwa njia ya
kielektroniki.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma, amesema zoezi hilo litasaidia kupata taarifa sahihi za watumiaji wa simu nchini.
“Sasa hivi zoezi litakuwa kiteknolojia zaidi. Utakuwa ukipigwa picha
na simu. Kwahiyo uso huwezi ukafeki,” amesema Profesa Nkoma.
Ameongeza kuwa zoezi hilo litasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa
udanganyifu uliopo kwenye matumizi ya simu nchini na hakutakuwa na
urahisi wa mtu kutumia jina la bandia pamoja na picha isiyokuwa yake.
Profesa Nkoma amesisitiza kuwa zoezi hilo halimaanishi kuwa ni
usajili mpya wa sim card bali ni uhakiki wa taarifa za watumiaji wa simu
nchini na linamhusu kila mmoja.
Kwa upande wake Rene Meza ambaye pamoja na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa
Vodacom Tanzania, ni mwenyekiti wa chama cha watoa huduma za mawasiliano
nchini, MOAT alisema zoezi la usajili wa simu nchini limeingia kwenye
hatua nyingine ya juu zaidi.
“Ni kwa kutumia teknolojia, na tena ni kwa smartphone ambayo wakala
wa usajili ataipata kwa si zaidi ya shilingi laki moja ambayo
itamsaidia kuchukua picha ya mteja anayetaka kusajili sim card yake.
Mchakato huo hautumia zaidi ya dakika tano,” alisema Meza.
Meza amesema usajili huo utafanyika nchi nzima na wameifanyia uhakiki
teknolojia hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu na tayari kuna vituo zaidi ya
5000 vinavyofanya usajili huo mpya.
Wateja watatakiwa kuonesha vitambulisho vinavyokubalika kufanikisha zoezi hilo na utagharimu shilingi 1000 tu.
Kwa upande wake mamlaka ya vitambulisho nchini, NIDA, imedai kuwa
vitambulisho vya uraia vitalazimika kutumika zaidi ili kupata taarifa
sahihi za watumiaji wa simu.
NIDA imesema imeboresha pia utoaji wa vitambulisho hivyo wa Dar es
Salaam ambapo wananchi wakiwasilisha viambatanisho vinavyotakiwa
watakuwa wakivipata ndani ya siku 7.

Note: Only a member of this blog may post a comment.