Pendo Madumu, aliyenusurika kifo baada ya kujifungulia nyumbani hapa akiwa amelazwa katika kituo cha afya Nguruka.
Akisimulia kisa hicho Justina Marko ambaye ni ndugu wa mwanamke huyo, alisema kuwa ndugu yake alitokwa na damu nyingi muda mfupi baada ya kujifungua na kuzidiwa hali iliyowalazimu kukodi pikipiki na kumkimbiza katika kituo cha afya cha Nguruka.
“Uchungu ameanza saa kumi na moja na saa kumi na mbili akajifungua, amejifungua mzima mpaka akaoga, akanywa na uji akakaa ndio akaanza sasa kutokwa damu tukaona sasa tukimbie kwenye hospitali; nguvu zote zilikuwa zimeisha mpaka tukaanza kumwagilizia maji,”alisema Justina.
Mtandao huu ulishuhudia mwanamke huyo akiwa amechubuka vidole vyake vya miguu kutokana kuburuza miguu yake chini wakati jitihada za kumfikisha kituo cha afya zikifanywa na ndugu zake.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Nguruka, Dr Stanford Chamgeni, ameeleza kuwa Aprili 6 mwaka huu walimpokea mwanamke huyo kituoni hapo hali yake ikiwa mahtuti baada ya kujifungulia nyumbani.
“Amejifungua kule kijijini akawa amepata mtoto vizuti na vitu vyote vikawa vimetoka vizuri kutoka tumboni, lakini amekuja hapa akiwa hajitambui kabisa,”alisema Dr Chamgeni.
“Tumeanza kumpa maji yanayohusika mikono yote miwili, tukampa dawa nyingine na sasa hivi yuko kwenye damu baada ya kupata maji.
Alipoanza kupata maji tu ya kutosha akawa maepata fahamu, lakini kama angekosa usafiri akakaa masaa mawili zaidi kwa kweli mama huyu alikuwa apoteze maisha.”
Aidha kutokana na kisa hicho, Dr Chamgeni ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha kwamba wanawahi kwenye vituo vya afya wakati wa kujifungua ili kuepuka vifo visivyo vya lazima.
“Sasa hivi kituo chetu kinajitahidi kutoa matibabu sahihi kwa wagonjwa wenye matatizo kama haya, kwa hiyo ni vizuri wawahi kuja kujifungua kituo cha afya,lakini kwa njia hii kama watu wataendelea kupenda kuwa wanajifungulia majumbani kuzuia kwake itakuwa ngumu sana.”


Note: Only a member of this blog may post a comment.