Friday, March 18, 2016

Anonymous

BARUA NZITO: Binamu, Zingatia Haya Jijini Daisalamu!

Leo asubuhi nimeletewa barua binamu yangu anataka kuja kunitembelea huku Daisalamu. Nimefurahi sana sijamuona siku nyingi, lakini ngoja nimuandikie barua ajitayarishe kisaikolojia na vituko vya Daisalamu.

Binamu yangu mpendwa,
vipi huko? Nimepokea barua yako ukiniambia unataka kuja Daisalamu kwa muda ‘kusafisha macho’. Binamu huku bwana watu wako bize sana na maisha ni magumu sana. Maisha ni magumu sana hivyo usishangae ukikuta mabinti wa huku wamevaa nguo zimechanikachanika wenyewe wanasema ni fashen japo habari za kuaminika ni kuwa panya wengi sana huku wanapenda kutafuna nguo.

Usishangae ukikuta mdada kavaa kakipande kadogo tu ka nguo, ni matatizo ya maisha yanamfanya alazimike kuvaa nguo alizokuwa akivaa wakati bado mdogo. Binamu naomba kisirani kiache hukohuko, watu wa huku wana maneno sana, kulima hawawezi lakini wanaweza kuongea mfululizo hata masaa manne.

Yaani huku hata kwenye redio kuna vipindi watu wanaongea masaa matatu mfululizo. Halafu binamu kuna jambo nisisahau, nimeona nikwambie kabla hujaja. Nimeona nigusie utaalam wa kuvuka barabara huku Daisalamu.
Najua kuna yale maelezo ya zamani kuwa ukitaka kuvuka barabara angalia kushoto, halafu angalia kulia, halafu angalia kushoto tena kisha vuka. Naomba nikwambie ushauri huo umepitwa na wakati, ukiufwata utavunjwa kiuno mapema huku Daisalamu.

Ukija huku kabla hujavuka barabara tafadhali fuata ushauri huu mpya. Kwanza kabla hujatoka nyumbani jaribu kupanga njia utakayopita, ikiwezekana kusiweko na kuvuka barabara, lakini ikilazimika, kabla ya kuvuka angalia kushoto na kisha angalia kulia halafu kushoto tena, halafu kulia tena, halafu kushoto halafu kulia, kisha sali sala zako za mwisho, baada ya hapo anza kuvuka taratibu maana hujui bodaboda au kibajaj kitaibukia wapi.

Kuna barabara moja inahitaji umakini wa kipekee, hii ni ile barabara ya njia tatu inayoanzia Bamaga hadi Moroko, ili kuvuka barabara hii fanya yote niliyokwambia hapo juu mara tatu, kisha funga macho muombe Mungu akutumie malaika wakuvushe halafu anza kuvuka. Binamu ukija nitakueleza mengine mengi.
Wasalaam
Chekana.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.