Mwimbaji nyota wa muziki wa Injili Bongo, Flora Mbasha.
Stori: Mayasa Mariwata
MCHUNGAJI Kongozi wa Kanisa la
Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na mwimbaji nyota wa muziki wa Injili
Bongo, Flora Mbasha watalazimika kumlipa mamilioni ya shilingi Emmanuel
Mbasha (33) kwa kitendo chao cha kumchafulia jina mbele ya jamii, Risasi
Mchanganyiko limeelezwa.
Hivi karibuni, Emmanuel ambaye ni mume
wa Flora, alishinda kesi ya ubakaji iliyofunguliwa dhidi yake katika
Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar akidaiwa kumbaka mdogo wa mkewe
waliyekuwa wakiishi naye nyumbani kwao, Tabata, Dar es Salaam, Juni
2014.
Katika shauri hilo, Mbasha alishitakiwa
na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (mlalamikaji anakuwa shahidi), kitu
kinachoibua maswali ni kwa namna gani Gwajima na Flora watahusishwa.
GWAJIMA, FLORA WANAHUSIKAJE?
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko
jijini Dar juzi, Mwanasheria na Ofisa wa Mahakama Kuu, Denis Maringo
alisema mazingira ya kesi hiyo iliyokuwa gumzo kubwa, yanawaingiza
wawili hao katika madai ambayo Mbasha anaweza kufungua kwani kuna
uhusiano unaojitosheleza kati yao na binti anayedai kubakwa.
“Inafahamika kwamba aliyedai kubakwa ni
mdogo wake Flora na kwa kipindi chote kile cha kesi, inafahamika pia
kuwa Flora alikuwa karibu na Mchungaji Gwajima, maana mara nyingi
zilisikika kauli za Mbasha kulalamika nyendo za mchungaji na mkewe.
“Kuna wakati Mbasha alidai kuwa,
alikwenda kwa Mchungaji Gwajima ili kupata muafaka wa tatizo lake na
mkewe, lakini akasema kiongozi huyo wa kiroho alimwambia kama mkewe
ameshaamua, ni vizuri akaheshimu uamuzi wake. Hii inaonesha ukaribu wa
wawili hao,” alisema mwanasheria huyo.
KWA NINI MBASHA ASHITAKI?
Mwanasheria huyo alisema kuwa, Mbasha
anaweza kufungua shauri la madai na kuomba fidia ya mamilioni ya fedha
kutokana na heshima yake kwa jamii kushuka na kuchafuka, hasa kwa
kulinganisha na umaarufu alionao katika jamii.
“Kesi ya ubakaji inamshushia mtu thamani
katika jamii, hivyo kutokana na adha hiyo, pale unapokutwa huna hatia
na mahakama unaruhusiwa kufungua kesi ya madai kwa lengo la kutaka fidia
kiasi unachokitaka na mahakama kukitolea uamuzi kwa kumshitaki mhusika
na wote walioshiriki katika kesi hiyo.
“Anachopaswa kufanya Mbasha ni kwenda
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ambayo ni tofauti na ile
ya awali iliyoendesha mashitaka na kufungua kesi ya madai ambapo sheria
ya mwaka 1971 inaruhusu mtu kufungua kesi ya aina hiyo kwa kipindi
kisichozidi miaka mitatu tangu hukumu itolewe. Kwa sababu ya
kudhalilishwa, atawashitaki waliomshitaki mwanzo kwa kesi ya jinai.”
SHERIA INASEMAJE?
Wakili huyo alichambua vipengele
vinavyompa urahisi Mbasha wa kufungua kesi hiyo kuwa ni kile kinachohusu
nia mbaya ya mfungua kesi akiwa na lengo la kumchafua.
“Mtu akikufungulia kesi kwa nia mbaya ya
kukuchafua wewe. Kwa hiyo, yeye na walioshirikiana naye, wote
wanahusika. Kipengele kingine ni kile cha adha ya kuwekwa ndani. Kwa
kuwa mahakama ilimkuta hana hatia, maana yake ni kwamba, kitendo cha
kuwekwa ndani ni cha uonevu unaoweza kuwaingiza matatani hata polisi
wenyewe.
“Jambo lingine linalompa nafasi Mbasha
ya kufungua madai ni kwa kitendo cha jamii kumuona tofauti kiasi kwamba
inaweza kumtenga kwa kuamini ni mbakaji. Ili kuwa fundisho kwa watu
wengine, anayo haki ya kudai fidia kwa kuchafuliwa jina kwani huenda
hiyo iliwafanya wahusika kunufaika kwa dhamira zao.”
Wakati ishu hiyo ikionekana kuwakalia
vibaya Mchungaji Gwajima na Flora, gazeti hili lilimtafuta Mbasha
ambaye baada ya kuelezwa kuhusu maelekezo ya mwanasheria huyo, aliomba
muda wa kutafakari pamoja na wanasheria wake.
“Ni kitu kipya unanieleza na kama
unavyojua hili ni suala la kisheria. Siwezi kulitolea maelezo mara moja,
inabidi kukutana na kushauriana na wanasheria wangu ili kuona nini
tunaweza kufanya,” alisema Mbasha.
Flora na Gwajima nao walitafutwa kupitia
simu zao za mkononi, lakini mara zote hazikuweza kupatikana hadi gazeti
hili lilipokwenda mtamboni. Hata hivyo, jitihada za kuwatafuta bado
zinaendelea.
Note: Only a member of this blog may post a comment.