Friday, June 12, 2015

Anonymous

KUMEKUCHA! Tambwe, Twite mzigoni!

Hans Mloli na Nicodemus Jonas
WACHEZAJI wa kigeni wa Yanga bado hawajatua nchini kwa ajili ya kuanza majukumu yao ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Kagame na Ligi Kuu Bara msimu ujao lakini imethibitika kuwa mshambuliaji hatari wa timu hiyo, Mrundi, Amissi Tambwe, atatua nchini kuanza kazi Jumanne ijayo.

Yanga ambayo imeanza mazoezi yake wiki hii kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar, imekuwa na mahudhurio ya wachezaji wachache kutokana na wengi wao kuwa na timu za taifa na wengine bado wapo mapumzikoni nchini kwao.

Tambwe amezungumza na Championi Ijumaa kwa kifupi moja kwa moja kutoka nchini kwao Burundi kulikokuwa na machafuko ya kisiasa ambapo amesema kwa sasa hali imetulia kidogo, hivyo anaweza kuondoka na kutua nchini mapema kuendelea na majukumu yake.

“Huku safi kidogo, mambo yanaonekana kutulia kidogo, tunamshukuru Mungu, angalau kwa sasa unaweza ukasema kuna unafuu, ila mimi nitakuja huko hivi karibuni tarehe 16,” alisema Tambwe aliyeifungia Yanga mabao 14, ndani ya mechi 18.
Nyota mwingine wa Yanga aliye mapumzikoni ni Mnyarwanda Mbuyu Twite ambaye taarifa kutoka kwa ndugu yake wa karibu aliyepo nchini zinafafanua kuwa atatua nchini pamoja na mkewe, Jumatatu ijayo akitokea kwao DR Congo.

Kwa upande wa Mliberia, Kpah Sherman, ambaye amekalia kuti kavu klabuni hapo, yeye amesema atatua nchini kesho Jumamosi au keshokutwa huku akitamba kwamba yupo tayari kuwaonyesha Wanayanga yeye ni nani, baada ya kuuanza msimu uliopita kwa kusuasua. “Ni kweli sikuwa kwenye kiwango changu, sikufanya vema kutokana na hali ya hewa ya joto ilinitesa sana. Ilikuwa mara ya kwanza kucheza sehemu ya joto jingi namna hii. Huko (Dar) nitakuja wikiendi hii, nimejiandaa vema baada ya kuizoea ligi na ninaamini nitafanya vizuri zaidi ya msimu uliopita, japo najua kuna ushindani mkubwa,” alisema Sherman.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.