MJOMBA WA MAREHEMU ASIMULIA
Akizungumza na gazeti hili mapema wiki hii juu ya mkasa huo wa
kusikitisha, mjomba wa marehemu Jagna, Ally Bilionea alisimulia kuwa,
marehemu alikuwa akiishi Mwembechai lakini hivi karibuni aliugua malaria
ndipo mkwewe, Amina akamtaka akaugulie kwake, Magomeni-Mikumi.
Mjomba mtu huyo alisema kwamba, wakati Jagna anaishi kwa mkwewe, mke
wake Jamila aliendelea kuishi Mwembechai japokuwa hawakuwa na
ugomvi.“Nakumbuka ilikuwa Jumatano ya wiki iliyopita. Nikiwa kwenye
shughuli zangu za ufundi wa magari, nilipokea simu kutoka kwa rafiki
yangu, akaniambia nyumbani kwa Jagna, Mwembechai kulikuwa na kilio.
“Ilibidi niende kule. Nilipofika, mke wa marehemu aliponiona alianza kuangua kilio akiniambia mumewe hajulikani alipo.
“Cha kushangaza, aliniambia Jagna alipotea saa moja iliyopita. Ilibidi nimuhoji inakuwaje aseme mtu amepotea kwa kutoonekana kwa muda mfupi kiasi hicho?
“Cha kushangaza, aliniambia Jagna alipotea saa moja iliyopita. Ilibidi nimuhoji inakuwaje aseme mtu amepotea kwa kutoonekana kwa muda mfupi kiasi hicho?
“Mkewe akasema kuna rafiki wa mumewe aitwaye Nairobi alimfuata Jagna
ukweni wakafanya biashara ya fedha nyingi na kuondoka naye kwenye gari
aina ya Toyota IST huku akiacha viatu vyake mlangoni,” alisema mjomba
huyo.
Akiendelea kueleza kwa majonzi makubwa, mjomba huyo alisema kuwa, Jamila
alidai kwa kuwa tangu Jagna ahamie kwa mkwewe hapo akiwa mgonjwa
(japokuwa si mgonjwa wa kulala kitandani), hakuwa na kawaida ya kutoka
ndiyo sababu iliyofanya aamini amepotea.
Mjomba huyo alisema ilibidi waanze harakati za kumtafuta kila kona ya
Jiji la Dar kuanzia kwenye vituo vya polisi, hospitali na mitaani
lakini bila mafanikio.
“Ilipofika Alhamisi, nilimwambia Jamila tukatoe taarifa Kituo cha
Polisi cha Magomeni. Baada ya hapo tulikaa kikao cha familia kujadili
jinsi ya kumpata ndugu yetu na hata tulipomuuliza Nairobi, alisema yeye
alifanya biashara na Jagna kisha akaondoka huku jamaa akirudi ndani kwa
mkwewe na kwamba, hakuondoka naye kama inavyodaiwa,” alieleza mjomba.
WAKUBALIANA KUCHUKUA POLISI
Alisema kuwa, baada ya kikao cha familia wakakubaliana siku iliyofuata (Ijumaa) wakachukue polisi, waende wakakague nyumbani kwa mkwewe alikokuwa akiishi Jagna kabla ya taarifa za kupotea.
SIKU YAFIKA
“Ilikuwa mishale ya saa moja asubuhi, Jamila alitoka chumbani huku akiongea na simu. Ghafla akaanza kulia na kuniambia Jagna amefariki dunia na maiti yake imekutwa kwenye kisima cha maji nyumbani kwa mama yake (Jamila).
“Tulipofika eneo la tukio, mimi niliwakuta kaka zake Jamila wakiwa katika zoezi la kuuopoa mwili wa Jagna kutoka kisimani. Wakati huo, Jamila yeye hakufika kuuthibitisha mwili wa mumewe badala yake alikwenda kwa ndugu wa mume kutaka awekwe eda. Mwili ulikutwa ukivuja damu.
MAJIRANI WATIA NENO
Kwenye eneo la tukio, baadhi ya majirani walioshuhudia tukio hilo walipozungumza na gazeti hili walidai kwamba usiku walisikia mtu akipiga kelele ndani ya ukuta wa fensi ya nyumba hiyo lakini hawakuwa na namna ya kuingia kujua kulikoni.
Mjomba huyo alidai kwamba, walipowauliza kaka wa Jamila kwa nini wasisubiri polisi wafike ndipo wautoe mwili huo walisema walikuwa wanamuonea huruma marehemu.
BABA MKWE AONA MAITI
Alisema walipoulizwa waliuonaje mwili huo, walijibu kuwa baba mkwe wa Jagna, Mzee Yusuf (si yule wa Jahazi Modern Taarab) ndiye aliyeuona wakati anachota maji.
“Baada ya hapo tukaenda kuchukua polisi ambao walikuja kuuchukua mwili kwa ajili ya vipimo na taratibu za mazishi huku ndugu wa marehemu wakilalamika kutopewa majibu ya vipimo hivyo.Hata hivyo, mama na baba Jamila, Jamila mwenyewe na kaka zake walikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Magomeni lakini mkewe aliachiwa siku iliyofuata huku simu zao zikishikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi.
SIKU CHACHE ALINUNUA NYUMBA
Ndugu upande wa marehemu walidai kwamba, Jagna alikutwa na mauti ikiwa ni siku chache tangu aliponunua nyumba maeneo ya Mwembechai yenye thamani ya Sh. milioni 80.
Habari kutoka ndani ya Kituo cha Polisi cha Magomeni zilieleza kuwa, kifo hicho kina utata mkubwa hivyo kinahitaji uchunguzi wa kina.
KAMANDA ANASEMAJE?
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Camilius Wambura alipoulizwa juu ya tukio hilo alisema kuwa halijamfikia mezani kwake hivyo ameahidi kulifuatilia kwa kina na kulipatia majibu.
Marehemu Jagna alizikwa Ijumaa iliyopita kwenye Makaburi ya Magomeni, Dar. Mungu ailaze mahali pema peponi, roho yake. Amina.

Note: Only a member of this blog may post a comment.