Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema akichaguliwa kuwa rais, hatamwogopa mtu wala hataacha mtu aonewe, hasa wanyonge.
Dk Magufuli alikuwa akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Zakhem, Mbagala.
Katika mkutano huo ulioandaliwa CCM
mkoani Dar es Salaam, Dk Magufuli alikuwa akitoa angalizo kila mara kuwa
hawezi kuzungumza sana kwa kuwa wakati wa kampeni haujafika, ingawa
katika hotuba yake fupi alitoa ahadi mbalimbali zenye sura ya kampeni.
Aliahidi kuwa atawashughulikia watendaji
wa Serikali ambao ni wazembe na kuhimiza utekelezaji wa ilani ya CCM.
Aliongeza kuwa hatamwonea haya mtu yeyote atakayekuwa kikwazo kwa
maendeleo ya Taifa.
“Mimi
siyo mkali, mimi ni mtu mpole sana lakini nawachukia watendaji wa
Serikali ambao ni wazembe, na hao ndiyo nitakao lala nao mbele,” alisema Dk Magufuli huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu waliohudhuria mkutano huo.
Dk Magufuli alisisitiza kuwa atasimamia
ilani ya chama ambayo imezingatia masuala ya kilimo na biashara. Alisema
ilani inawalinda wafanyabiashara wadogo na wakubwa, pia kuongeza fursa
za ajira kwa vijana.
“Maendeleo
hayana chama lakini maendeleo ya kweli yataletwa na CCM. Wakati wa
uchaguzi ukifika mchague wabunge na madiwani wa CCM ili kukamilisha
mafiga matatu,”Magufuli.
“Ukiwa
na tochi inayotumia betri tatu, wewe ukaweka betri mbili halafu
katikati ukaweka gunzi, hiyo tochi itawaka?” Dk Magufuli aliuliza
makutano ambao nao walimjibu kwa pamoja “haiwaki”.
Dk Magufuli, ambaye ni Waziri wa Ujenzi,
aliwashukuru wananchi kwa mapokezi makubwa aliyoyapata kuanzia Uwanja
wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) hadi viwanja vya Zakhem, Mbagala.
Alisema yeye na mgombea mwenza
watahakikisha wanalipa fadhila kwa vitendo, endapo watashinda Uchaguzi
Mkuu ujao na kuongoza Serikali.
“Ninawashukuru
wakazi wa Dar es Salaam kwa kuweka pembeni kambi zenu na kujitokeza
kutupokea wagombea wenu. Tulikuwa wagombea 42 wenye sifa sawa, na kila
mmoja alikuwa na kambi yake. Kuwa na kambi siyo kosa. Lakini wote
wamevunja kambi zao na kuniunga mkono ili kukipa ushindi Chama cha
Mapinduzi,” alisema.


Note: Only a member of this blog may post a comment.