Wednesday, June 3, 2015

Anonymous

YANGA SC JEURI: Sasa Yatua kwa Mu-Ivory Coast WAWA

Beki wa Azam, Paschal Serge Wawa.
Waandishi Wetu, Dar es Salaam
AMA kweli sasa Yanga imeamua kufanya yake bila ya kumuangalia mtu usoni baada ya kugonga hodi Azam FC na kuulizia huduma ya beki wake wa kati mwenye kila sifa ya kumudu majukumu yake uwanjani na roho ya ulinzi ya timu hiyo, Muivorycoast, Paschal Serge Wawa.

Yanga imefikia hatua hiyo baada ya kuwepo kwa shinikizo la kocha mkuu wa timu hiyo, Mdachi, Hans van Der Pluijm, aliyemjumuisha Wawa kwenye ripoti yake ya usajili ya mwisho wa msimu na kusisitiza kuwa ili Yanga iwe salama kwenye safu ya mabeki msimu ujao ni lazima aletewe mchezaji huyo.

Mmoja wa viongozi wa juu wa Yanga kwa sharti la kutotajwa jina gazetini ameliambia Championi Jumatano kila kitu juu ya mpango huo ambao tayari maombi ya awali juu ya kumnyakua Wawa yameshawasilishwa Azam.

Imeelezwa kwamba japokuwa Yanga imeamua kujitosa na kuzungumza na Azam juu ya suala hilo, lakini wasiwasi uliopo ni juu ya dau watakalopewa kwa ajili ya kukamilisha dili la beki huyo wa zamani wa El Merrikh ya Sudan anayetajwa kulipwa hela nyingi kuliko wachezaji wote hapa Bongo na Wanalambalamba hao.

Chanzo hicho kimeongeza kuwa hata wakati Kocha Hans Pluijm alipowasilisha kuachwa kwa Kelvin Yondani, alikuwa na ‘target’ hizo za Wawa, lakini baada ya kukaa na kujadiliana baadhi ya vitu na kamati husika, ndipo akawa mpole na kusubiri matokeo ya zoezi hilo linaloonekana kuwa gumu kwa wapenzi wengi wa soka nchini.

“Ngoja nikwambie kitu, unajua kwa sasa kuna usajili wa mchezaji mmoja unatusumbua kidogo kichwani, Pluijm anamtaka Wawa na hili amekuwa akiliongea lakini sasa amelisisitiza mpaka kwenye hii ripoti yake ya mwisho ya usajili.

“Huwezi amini hata lilipotokea suala la kuachwa kwa Yondani, target kubwa ilikuwa ni kwa Wawa ndiyo awe mrithi wake lakini tukakaa na kujadiliana na mwalimu kwanza na kilichomuokoa Yondani ni ile ‘performance’ yake kwenye mechi za mwisho na hata kitabia pia amebadilika na kuanza kukaa kwenye mstari anaoutaka kocha,” alisema kigogo huyo na kuongeza:

“Tayari tumeanza mazungumzo na Azam kwa ajili ya kuona kama wanaweza kutuachia Wawa lakini bado tunasikilizia dau watakalotutajia, maana kama unavyojua Wawa ni mchezaji wa kariba ya tofauti na kazi yake uwanjani kila mmoja anaijua halafu bado ana mkataba halali na Azam tunasikia mshahara wake ni dola elfu 10 (zaidi ya milioni 19) hivyo ni ngumu lakini tutapambana.”

Baada ya taarifa hizo nyeti, alitafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Yanga, Jerry Muro, kwa ajili ya kulitolea ufafanuzi suala hilo ambapo alishindwa kukanusha wala kukubali uwepo wa suala hilo na kusema machache.
“Siwezi kusema lolote kwa sasa, mambo ya usajili bado yanaendelea na hatuwezi jua nini kilichopo mbele yetu na kama kungekuwa na lolote basi mngeshapewa taarifa,” alisema Muro.

Alipoulizwa juu ya suala hilo Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba alisema; “Kwanza kama wanamtaka, wanajua hatua wafike kwetu sisi tutawaambia kama mchezaji anauzwa ama la, kwetu hawajafika.

Kwa kifupi ni kwamba Wawa hayupo sokoni na ni mchezaji wa Azam,” alisema Kawemba na kufunguka kuhusu iwapo Yanga watakuja na dau nono:
“Wawa sio Busungu (Malimi), hana shida ya hela, siku zote hakuna mchezaji wa Azam mwenye shida ya hela. Lakini pia kama wanamtaka, mbona kuna akina Wawa wengi huko nje, si wakachukue huko? Alihoji Kawemba.”

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.