Erick Evarist WAKATI wagombea
mbalimbali wa urais wa Tanzania wakitangaza nia ya kushika wadhifa huo
mzito kwa taifa, nyuma ya mchakato huo kumeibuka mpasuko mkubwa kwa
mastaa wakipigana vikumbo kuwania kambi za wagombea.
Kwa mujibu wa chanzo kilicho karibu na mastaa hao, mpasuko
umejidhihirisha hadharani Jumamosi iliyopita baada ya baadhi ya mastaa
kupata shavu la kwenda kutumbuiza katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid
Kiluta wakati Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa
alipokuwa akitangaza nia.
“Mastaa wamegawanyika. Wale waliopata bahati ya kwenda kama kina
Dully Sykes, Tunda Man, Khadija Kopa, Nay wa Mitego wameibua minong’ono
kwamba kuna fitina wamefanya ili wenzao wakose nafasi hiyo waneemeke
peke yao. Waliokosa nafasi nao wamejiunga na kuanza kutafuta kambi kwa
mgombea mwingine,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilizidi kueleza kuwa, mastaa kama Judith Wambura
‘Jide’, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’, Vincent Kigosi ‘Ray’ na Jacob
Steven ‘JB’ wao walifanya fitina kivyao na kufanikiwa kuinasa kambi ya
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wasira ambaye alitangaza
nia ya kuwania urais Jumapili iliyopita kwenye Ukumbi wa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) jijini Mwanza.
Wasanii hao walipopigiwa simu na kuulizwa kuhusiana na mpasuko huo,
walidai hawaoni kama ni tatizo kutofautiana kwa kipindi hiki cha
kuelekea kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka
huu kwani ndiyo siasa ilivyo.
“Wewe acha tutofautiane kisiasa lakini
zikipita tunarudi kwenye mstari mmoja kwani mashabiki wetu ukishapita
uchaguzi wanasahau,” alisema mmoja wa wasanii hao aliyeomba hifadhi ya
jina.

Note: Only a member of this blog may post a comment.